Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikijitosheleza kwa uzalishaji wa umeme, tatizo la kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo, ni kilio cha baadhi ya wananchi wanaoleleza kutonufaika nao, huku wakipata hasara kutokana na vifaa kuungua.
Wananchi wamekuwa wakitoa vilio vyao
kupitia makundi sogozi ya WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii, ikiwemo ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), wakati huohuo, lenyewe kwa nyakati tofauti likieleza kuwa changamoto hiyo inatokana na miundombinu.
Mbali na miundombinu, Tanesco limeeleza katika siku za karibuni, kimbunga Dikeledi kimekuwa tatizo kwa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani Lindi na Mtwara.
Desemba, 2024 akizindua mradi wa usafirishaji umeme wa kilovoti 400 Chalinze-Dodoma na upanuzi wa vituo vya umeme Chalinze na Zuzu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko alisema jitihada za kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme nchini zimewezesha kuongeza uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyopo nchini hadi kufikia megawati 3,169.26.
Alisema mahitaji ya juu ya umeme nchini kwa sasa yamefikia megawati 1,888.72 ambayo hayajawahi kufikiwa.
Alisema kuimarika kwa uzalishaji wa umeme kumechangiwa na kuanza uzalishaji katika mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 na kwamba, megawati 1,175 za umeme zinazalishwa na kuingizwa kwenye Gridi ya Taifa.
Akizungumza na Mwananchi, Mohammed Issa, mfanyabiashara ya chakula jijini Dar es Salaam amesema kukatika umeme mara kwa mara kumesababisha asiwe na uhakika wa kuhudumia wateja kwa wakati.
“Tena afadhali jioni siyo mchana, hadi chipsi zinakauka umeme unaweza kukata mara tatu mwisho unaamua kutumia gesi ili usipate hasara ya kuunguza vifaa,” amesema mwananchi huyo anayefanya biashara eneo la Tabata.
Kupitia ukurasa wa Instagram wa Tanesco, @officialrobby_255 aliandika kuwahoji Tanesco iwapo wanajua umeme si wa uhakika, wakate kwa muda mrefu wafanye maboresho ndipo waurudishe kwa wananchi.
“Wakuu kama mnajua umeme wenu sio wa uhakika tafadhali kateni umeme moja kwa moja fanyeni marekebisho halafu mtupe umeme ulio na uhakika na sio kama hivi mnavyotufanyia Kinyerezi Msikitini njia ya kwenda Bonyokwa…”
Amesema kutokana na changamoto hiyo ya umeme, runinga na kiyoyozi vimeungua na kwamba sasa anaogopa kutumia vyombo vya umeme kwa kuhofia kupata hasara.
Mteja mwingine wa shirika hilo alihoji akiesema Kimara Suka kwa wiki ya pili sasa unakatika asubuhi na kurejea saa nne au saa tano akitaka maelezo.
Msemaji wa Tanesco, Kenneth Boymanda alipotafutwa na Mwananchi leo Januari 16, 2025 amesema kukatika ovyo kwa umeme katika baadhi ya maeneo tangu Jumatatu (Januari 13) kumesababishwa na kimbunga Dikeledi.
“Tangu Jumatatu, mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na mikoa ya kusini ikiwemo Lindi imekuwa na tatizo hili, TMA (Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania) ilitoa tahadhari ya kimbunga Dikeledi, hakijawa na madhara makubwa kwenye maeneo mengi ikiwemo kwenye makazi ya watu.
“Lakini kulikuwa na upepo mkali na kama unavyojua miundombinu ya Tanesco iko juu hivyo imekuwa ikiathiriwa,” amesema.
Januari 14, TMA ilitoa taarifa ya uwepo wa kimbunga hicho katika Bahari ya Hindi mwambao wa pwani ya Msumbiji.
TMA ilieleza kuhusu matarajio ya uwepo wa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa ya bahari kwa maeneo ya ukanda wote wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo jirani hususani kati ya Januari 14 na 15.
Hata hivyo, taarifa ya tahadhari ya uwepo wa vipindi vya upepo mkali na mawimbi makubwa mamlaka ilianza kuitoa Januari 11, 2025. Ilisema hali ya upepo inatarajiwa kuwa shwari kuanzia leo Januari 16.
Boymanda amesema upepo ulikuwa ukisababisha miundombinu kuathiriwa ikiwemo kuangukiwa na matawi ya miti yaliyosababisha nyaya kuchapana (kugusana) na kuathiri usafirishaji umeme.
“Kuanzia leo (Januari 16) upepo mkali umeanza kupungua na hali imeanza kurejea katika hali yake ya kawaida, hakukuwa na uharibifu wa moja kwa moja zaidi ya miti inayoangukia nyaya,” amesema.
Novemba 8, 2024 Mwananchi iliripoti pia kuhusu katikakatika ya umeme, malalamiko yaliyotolewa na wakazi wa maeneo ya Kimara, Goba, Mbezi, Mbagala na Majohe.
Ashura Abdallah, mkazi wa Kimara Saranga alisema kwa takribani siku tano walikuwa wakikata umeme mara kwa mara hasa inapofika nyakati za usiku na wakati mwingine umeme hukatika katika baadhi ya nyumba na nyingine zikiendelea kupata huduma hiyo.
“Ukikatika unaweza kuchukua takribani dakika 30 hadi saa moja kurudi na kwa siku huweza kukatika zaidi ya mara moja,” alisema.
Kwa wakati huo, Boymanda alisema hali hiyo ilisababishwa na hitilafu katika miundombinu ya usambazaji umeme katika baadhi ya maeneo katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwemo Tabata, Goba na njia zinazohudumia ukanda huo.
“Zipo hitilafu ambazo zilitokea, ikitokea katika eneo fulani kutokana na ukubwa wake inaweza pia kuleta athari katika maeneo mengine, hivyo inaweza kupelekea kutibu eneo hili leo kesho ikajitokeza mahala pengine.
“Ni hitilafu ambazo zinaweza kutokea na timu zetu katika maeneo hayo yaliyopata changamoto zinaendelea kufanya kazi usiku na mchana kwa haraka ili kuzidhibiti zisiendelee kujitokeza,” alisema.
Mtaalamu wa Uchumi na Biashara, Dk Balozi Morwa amesema uwepo wa umeme muda wote unampa uhakika mzalishaji kutengeneza bidhaa kwa muda aliopanga, kinyume chake ni kuhatarisha uchumi kwani hawatakuwa na bidhaa walizozalisha na kuziuza, hivyo Serikali itakosa kodi kwa kiwango ambacho ilipaswa kulipwa.
“Watu kama wauza samaki, watu wa saluni, unamkatia umeme wakati mwisho wa mwaka unataka kodi, apate wapi kodi hapa ndiyo wanaanza kukimbiakimbia,” amesema.
Amesema kukatika umeme na kusababisha matumizi ya jenereta pia kunasababisha uchafuzi wa mazingira kwenye hewa na kuleta kelele.
“Jambo hilo pia linachangia kukatisha tamaa wawekezaji kwani wanashindwa kuwekeza katika mazingira ambayo hawana uhakika wa nishati ya kuzalisha bidhaa,” amesema.