Dar es Salaam. Kukithiri kwa vitendo vya rushwa nchini kunatajwa kuwa tatizo mtambuka linalogusa malezi, kukosa hofu ya Mungu, na ukosefu wa masilahi kazini.
Hayo yanaelezwa kutokana na video iliyosambaa mitandaoni, ikiwaonyesha askari polisi wawili wa usalama barabarani wakichukua vitu vinavyodaiwa kuwa fedha kutoka kwa madereva na makondakta wa daladala jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Januari 15, 2025, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, alisema wamewakamata askari hao kwa kuwa wamefanya vitendo visivyo vya maadili ambavyo vinachafua taswira ya Jeshi la Polisi.
Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi leo Januari 16, Kamanda Muliro amewaonya madereva wanaotoa rushwa kwa trafiki, akisema wao ndio chanzo cha kuchafua polisi.
Wadau wakiwemo wanasaikolojia na viongozi wa dini, waliozungumza na Mwananchi, wamesema tatizo la rushwa limekita mizizi kwenye malezi.
“Rushwa imekuwa maradhi kwa jamii, na ili iishe ni lazima kwanza jamii iichukie. Unakuta baba anamwambia mtoto, ‘ukifanya hivi nitakupa zawadi’, kwa hiyo anakua akijua kila atakachofanya lazima apewe zawadi. Hivyo, watu wanakua wakijua hata kutoa huduma fulani lazima umpe chochote.
“Kwa hiyo, vita vya rushwa vinapaswa kuanzia kwenye familia kwa kuwekeza kwenye malezi,” amesema Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka.
Askofu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God, Zanzibar, Dickson Kaganga, amesema ni lazima jamii ifahamu rushwa ni dhambi kama zilivyo nyingine, hivyo wawe na hofu ya Mungu.
“Biblia inasema rushwa inapofua macho, pale anapopaswa kuona anaweza asione, rushwa inaweza kumtoa muuaji na ikamuhukumu mwingine, unaweza kukuta watu wamefungwa lakini si kweli kwamba walikuwa na kosa,” amesema.
Amesema jukumu la viongozi wa dini ni kuwaelimisha waumini kuwa rushwa ni dhambi kama nyingine zozote.
“Mtu anapotoa rushwa anatenda dhambi, anamkosea Mungu,” amesema.
Mwanasaikolojia Jacob Kilimba amesema ugumu wa maisha umewafanya watu washindwe kulinda heshima na utu wao kwa kujiingiza kwenye vitendo vya hatari.
“Mtu hafikirii nje ya boksi kwa haraka, kwamba labda aanzishe biashara anaona itachukua muda mrefu, ndiyo anaingia kwenye vitu vya hatari kama rushwa, kubeti na mambo kama hayo kuliko kusubiri mchakato wa kimaisha,” amesema.
Ameshauri watu wajifunze kuishi na shida na kwa viwango walivyonavyo.
“Katika ulimwengu wa sasa wa teknolojia, huwezi kujua nani kamweka nani, hujui nani anakuchukia, nani anakupenda, hujui nani anakurekodi umechukua Sh1,000 tu, unaweza kuhatarisha maisha yako au ukapoteza kazi kwa sababu ya vitu vidogo. Tujifunze kuwa wavumilivu hasa unapopungukiwa, shida haziishi,” amesema.
Suala la rushwa limeibuka ikiwa imepita miezi sita tangu Mwananchi lilipofanya uchunguzi na kubaini madereva na makondakta wa daladala wamekuwa wakitoa fedha kwa trafiki.
Uchunguzi huo uliochapishwa Julai 2024, ulibaini madereva hutakiwa kuwalipa wamiliki wa magari kati ya Sh80,000 hadi 200,000 kama hesabu ya siku. Pia hutenga hadi Sh20,000 kwa ajili ya kutoa kwa trafiki kila wanapokamatwa.
Utafiti uliotolewa na Shirika la Twaweza East Africa, Novemba 2017 ulionyesha licha ya kupungua kwa vitendo vya rushwa wakati huo, taasisi zilizotajwa kuongoza katika rushwa ni Polisi na Mahakama.
“Licha ya maboresho katika maswali kwa wananchi kuhusu rushwa, wanasema polisi na mahakama bado zinaongoza, ambapo asilimia 39 na 36 ya wananchi wanasema waliombwa rushwa katika mawasiliano yao ya mwisho na taasisi hizi mbili.
“Hata hivyo, chini ya asilimia 20 ya wananchi waliripoti kuombwa rushwa mwaka 2017 katika sekta nyingine, zikiwemo ardhi (asilimia 18), afya (asilimia 11) na maji (asilimia 6).
Ripoti nyingine iliyotolewa na taasisi ya Afrobarometer Januari 2024 iliyofanya uchambuzi wa majeshi ya polisi barani Afrika kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2021 hadi 2023, polisi imetajwa kuwa taasisi inayoongoza kwa rushwa Afrika, ikifuatiwa na wabunge.
Wengine ni maofisa wa kodi, watumishi wa umma, ofisi za marais, watendaji wa biashara, majaji na Mahakama, serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali, viongozi wa jadi na viongozi wa dini.
Katika majeshi ya polisi, polisi wa Uganda wameongoza, wakifuatiwa na Nigeria, Sierra Leone, Gabon, Kenya, Liberia, Ghana, Afrika Kusini, Cameroun na Msumbiji, huku Tanzania ikishika nafasi ya 32.
Baadhi ya trafiki waliozungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa majina wamesema tatizo siyo mshahara kidogo au kutokuwa na mishahara minono, bali ni ushawishi kutoka kwa madereva.
“Siyo kama shida ni mshahara, japo mshahara huwa ni siri ya mtu, lakini kwa hiki kinachoendelea shida inaanzia kwa madereva,” amesema mmoja wa askari hao.
Amesema trafiki anapomkamata dereva kwa kosa kama la kupita gari lingine sehemu isiyoruhusiwa ama amezidisha mwendo au hajafunga mkanda na dereva huyo ni kweli amefanya kosa hilo, anapokamatwa anatakiwa aandikiwe faini ya Sh30,000.
“Hii faini utailipa kwa hiari ndani ya siku saba, lakini inapofika trafiki anamuomba leseni, anapaswa kumpa ili amuandikie faini na si kumtengenezea mazingira ya kumhonga,” amesema.
Amesema hakuna trafiki anayemuomba dereva pesa baada ya kumkamata, madereva ndio wanatengeneza mazingira hayo.
“Ingekuwa kwenye nchi za wenzetu kule wana mfumo, mfano ukipita kwenye zebra (alama ya pundamilia) hujasimama, faini inaingia moja kwa moja.
“Hapa kwetu unamkamata dereva anaanza kukuomba msamaha au kukwambia ana dharura, kwa wenzetu huwezi kusema ‘nisamehe’, umefanya kosa unapigwa faini moja kwa moja,” amesema.
Trafiki mwingine amesema changamoto kubwa barabarani ipo hasa kwa madereva wa daladala.
“Kuna wanaopakia au kushusha abiria sehemu ambayo haina kituo ni kosa, lakini kibinadamu unaona ukimuandikia faini ya Sh30,000 wakati abiria huyo analipa nauli Sh600 ni kumrudisha nyuma huyo dereva, tunajaribu kuwaelimisha lakini hawasikii ndipo wanatengeneza mazingira ya rushwa,” amesema.
Kamanda Muliro akizungumza na Mwananchi amesema madereva wanaotoa rushwa ndio wanaolichafua Jeshi la Polisi.
“Tunahitaji nidhamu kwenye Jeshi la Polisi na wananchi kuacha kulichafua. Hao trafiki wanazichukua pesa kutoka wapi, si kwa madereva? Ni kwa nini wanatoa hizo pesa? wana uhalali wa kutoa?
“Kwa nini watu hawawashambulii madereva wanaotoa? Nasema nataka tuanzie hapo, wale nao wanatuaibisha sana na wananchi wamekubaliana na huo uchafu, sasa nikimbaini dereva anayetoa rushwa kwa trafiki, adhabu yake itakuwa kubwa kushinda ya huyo trafiki aliyepewa rushwa,” amesema.
Hata hivyo, madereva waliozungumza na Mwananchi wametofautiana na polisi.
“Binafsi naona ni sawa, kuliko kulipa elfu 30, bora nimpe trafiki Sh5,000,” amesema Juma Shaban wa Kibaha.
Mussa Mhando amesema, trafiki anapokukamata hata kama gari liko vipi hawezi kukosa kosa.
“Wakati mwingine tunakimbilia kuwapa pesa ili kuepusha mambo mengine na faini kubwa, lakini kama huna kosa au amekukuta na kosa dogo kama umesahau kufunga mkanda, akuelimishe tu,” amesema.
Eliya Deus amesema changamoto ya yote hayo ni trafiki wenyewe.
“Mfano mdogo ni kwenye stika za nenda kwa usalama, ili uipate gari lako linatakiwa likaguliwe, lakini si kila gari lenye stika limekaguliwa,” amesema.
Juhudi za kumpata Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Crispin Chalamila hazikufanikiwa, baada ya simu yake kutopatikana.
Hata hivyo, akizungumza katika kipindi cha rushwa adui wa haki kinachorushwa na TBC, mwanzoni mwa mwaka huu, Chalamila alisema mwaka huu ambao utakuwa na uchaguzi mkuu, wamejipanga kuzuia na kupambana na rushwa kwa kasi kubwa.
“Tunajua vitendo vya rushwa kwa jumla huwa vinaibuka wakati huu wa kuelekea kwenye uchaguzi, kwa hiyo tunawaomba watoe ushirikiano wa taarifa za vitendo hivyo,” amesema.
Imeandikwa na Elias Msuya, Imani Makongoro na Elizabeth Edward.