Kila mtu ni mstaafu mtarajiwa anayepaswa kuyafanyia kazi yanayomhusu yeye na wastaafu wenzake anaowaona leo watakaokuwa wenzake kesho, waweze kustaafu salama salimini wakiwa na amani.
Yasije yakawa mambo ya kulazimika kusubiri miaka 20 baada ya kustaafu kwake ili kupata nyongeza ya shilingi elfu hamsini kwenye ‘laki si pesa’ yake aliyokuwa akipokea. Siyo agizo wala sheria iliyowekwa na mitume au malaika bali Mmatumbi mwenzetu huyu huyu.
Ndiyo, hili siyo agizo lililotoka kwa mitume au malaika, wala siyo amri ya kumi na moja kwamba mwajiriwa akishastaafu akae miaka 20 kwanza na pensheni yake ya ‘laki si pesa’ ndiyo apewe nyongeza.
Tukumbuke kwamba zile amri kumi za Mungu zinavunjwa kila uchao na uchwao. Watu siyo tu kwamba huoneana wivu bali hata kuuana, mbali na kumtumbulia macho mume au mke wa mwenzao, pamoja na kuwa imeandikwa wazi kuwa ukifanya hivyo unakuwa tayari umefanya ‘vitu vyako’ naye, na itakupasa hukumu.
Na hapo usitaje ile amri inayokataza watu kuiba, kwani sasa wanaiba kama hakuna kesho. Kila mtu sasa akiwa bize kuchukua chake mapema, sijui ili awahi wapi? Tofauti na ushauri tunaopewa kwenye dini zetu kwamba kwenye matendo yetu hata mkono wetu wa kulia usijue wa kushoto unafanya nini, kwenye kuhomola kwetu siku hizi mikono yote miwili inahimizana kuiba! Na ‘wanachori’ kweli, kama CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) anavyotuambia kila mwaka. (Kiponjoro ili kuweka msisitizo).
Mara kwa mara, mstaafu wetu hujikuta akikumbuka hadithi ya mzee wake mmoja aliyekuwa miongoni mwa wastaafu wa mwanzo kabisa wa nchi hii akiwa mwajiriwa wa kule ‘jikoni’ kabisa kwa uongozi wa nchi. Hiki kilio cha wastaafu kuwa mishahara midogo na pensheni ndogo hakikuanza leo. Kimekuwepo tangu tulipolazimika kuanza kukaza mikanda baada ya vita ya Kagera. Ni kwa vile tu waajiriwa wa wakati huo walikuwa na uzalendo na nidhamu, kilio chao kikawa siri.
Huyu mzee wetu akiwa kule ‘jikoni’ kabisa mwa utawala wa nchi, kule ambako kauli yake tu ingeweza kutingisha watu, waajiriwa wa wakati huo wakawa wakimzukia ofisini kwake kumuomba afanye kila awezalo ili mishahara ya waajiriwa na pensheni ya wastaafu iongezwe, maana ilikuwa ni ndogo isiyoendana na maisha ya wakati huo. Pamoja na kwamba watu waliweza kununua redio ya National ya ‘Mkulima ya mbao ya Dudu Proof’ kwa shilingi 380, kupata hizo shilingi 380 ilikuwa shughuli.
Inawezekana kwa kujiona bado kijana na akifanya kazi ‘jikoni’ kabisa mwa uongozi wa nchi na mshahara wake, marupurupu na marapurapu yake yakiwa si haba, akawa akitia kapuni tu kilio cha waajiriwa wa nchi cha kutaka mishahara iongezwe ili pensheni yao ieleweke. Aliwaambia wasipende sana hela bali wakazane kufanya kazi ili hela zipatikane zaidi. Akawa kama aliyeshiba asiyewakumbuka wenye njaa.
Kila mtu ni mstaafu mtarajiwa, kama Mungu hajamharakisha Kinondoni akiwa bado mwajiriwa kijana. Umri ukasonga mbele, na mzee mstaafu akalazimika kustaafu kama sheria inavyomtaka. Akiwa na miaka 60, akalazimika ‘kuachia ngazi mchuma uondoke’. Ndipo akajua kwa nini waajiriwa walikuwa wakimsumbua wakimtaka aongeze mishahara, huku yeye akiuchuna tu!
Wakati akiwa kule ‘jikoni’, alikokuwa na madaraka, akipiga kofi tu analetewa chai ya maziwa na mkate wa siha wenye siagi na jam, akimalizia kwa kishushio cha juisi bila kutoa hata thumni. Huku mitaani, ambako wastaafu wenzake waliompigia kelele aongeze mishahara walikuwa wameizoea hiyo hali, alilazimika kutoa shilingi kadhaa kila asubuhi ili familia yake ipate vitumbua vya kuitosheleza.
Haikuchukua muda kabla hali ya mzee mstaafu kuwa siyo njema huku shinikizo la damu likifanya ‘vitu vyake’ vya kushinikiza damu. Magonjwa ya kiutu uzima yakamfanya mzee wetu sasa atamani kurudi kule alikokuwa akifanya kazi, apandishe mishahara kwa hasira ili pensheni za wastaafu zieleweke. Lakini ndiyo, alikuwa ameishachelewa, mchuma ulikuwa umepuyanga!
Historia ina kawaida ya kujirudia. Mstaafu wetu anapenda kudhani kwamba hata suruali ya ‘Pekos’ aliyotamba nayo miaka ile ya ujana wake na viatu vya Gudile ‘Raizon’ (rise on) kuna siku vitarudi mitaani. Ameshaona nywele za Afro mbili, tatu mitaani. Vitarudi. Kila mtu ni mstaafu mtarajiwa. Kwa busara za kawaida kabisa, anatakiwa akifanya kazi mahali anapaswa kuyafanyia kazi yale yote anayoona yatamsaidia yeye na wastaafu wenzake kuboresha maisha yao baada ya kuitumikia nchi.
Hapaswi kuona wastaafu wa nchi wanakaa miaka 20 bila nyongeza ya pensheni na kuwa na amani wakati yupo mahali ambako anaweza kupiga kelele na ikasikilizwa. Asiishie kuona mstaafu akipata nyongeza ya shilingi elfu hamsini baada ya miaka 20 na akaridhika wakati uwezo wa kukemea hili anao, kama maisha ya mstaafu hayamhusu. Yanamhusu. Yeye ni mstaafu mtarajiwa. Atayakuta haya, ndipo atajikuta akilia na kuomboleza, akitamani awe kazini apandishe pensheni kwa hasira lakini atakuwa ameishachelewa na mchuma umepuyanga.