Kocha Amrouche yu wapi? | Mwanaspoti

ADHABU ya mechi nane alizoadhibiwa Kocha Mkuu wa timu ya taifa, Taifa Stars, Adel Amrouche kwa kosa la kutoa shtuma nzito dhidi Shirikisho la Soka la Morocco (RMFF) ni kama imeisha, lakini kumekuwa na ukimya juu ya hatma ya kocha huyo ndani ya kikosi hicho cha timu ya Tanzania.

Kocha huyo raia wa Algeria aliadhibiwa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Januari 18, mwaka jana mara baada ya Stars kupasuka mabao 3-0 mbele ya Morocco katika mechi ya kwanza ya makundi ya Fainali za Afcon 2023 zilizofanyika mwaka jana huko Ivory Coast kabla ya kutoa kauli zinazodai RMFF ina ushawishi ndani ya CAF ya kupanga mechi na waamuzi.

Kitendo hicho, kilisababisha Kamati ya Nidhamu ya CAF kumfungia mechi hizo nane na kumlima faini ya Dola za Kimarekani 10,000 ( shilingi 24 milioni) pia Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), nayo ilitangaza kumsimamisha kocha huyo Januari 19, kama kuungana mkono hatua ya CAF na kumpa kazi Kocha Msaidizi, Juma Mgunda kumalizia mechi za mwisho za makundi dhidi ya Zambia na DR Congo.

Baada ya mechi hizo mbili za fainali za AFCON, Stars ilicheza mechi nyingine sita za kuwania AFCON 2025 na kufuzu ikiwa chini ya Kaimu Kocha Mkuu, Suleiman Hemed ‘Morocco’ mbali na zile za kuwania fainali za Kombe la Dunia za 2026 na kukamilisha idadi ya mechi ambazo kocha Amrouche aliadhibiwa na CAF.

Licha ya mechi hizo nane kukamilika, hadi sasa TFF haijawahi kutoa kauli yoyote juu ya kocha Amrouche kwani shughuli za timu za taifa zinaendelea kufanywa na Morocco, jambo lililoanza kuibua mijadala kwa wadau wa michezo juu ya hatma ya kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars ya Kenya.

Hata hivyo, Mwanaspoti  limewasiliana na Ofisa Habari wa TFF, Cliford Ndimbo na kuulizwa kuhusu hatma ya Amrouche aliyeajiriwa na TFF Machi, 2023 kwa mkataba wa miaka mitatu ambao unatarajiwa kumalizika mwakani, huku ikielezwa mshahara wake unalipwa na serikali, ambapo alisema itatolewa taarifa rasmi.

“Kwa sasa siwezi kusema lolote, suala la kocha Adel (Amrouche) litatolewa taarifa rasmi,” alisema Ndimbo.

Related Posts