Lissu ataka Bawacha kupigania mageuzi

Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu amelitaka Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha) kupigania mabadiliko ili kupata uwakilishi wa wanawake kwa usawa kwenye vyombo uamuzi.

Amesisitiza Chadema inahitaji viongozi wa kupigania mabadiliko na wanaojua bila mabadiliko hayo idadi ya wanawake bungeni haitoongezeka.

Lissu ametoa kauli hiyo leo Januari 16, 2025 Dar es Salaam wakati wakitoa salamu zake kwa Bawacha katika mkutano mkuu wa baraza hilo ambalo leo linafanya uchaguzi wa nafasi mbalimbali za uongozi kitaifa.

“Kwa hiyo kwenye uchaguzi huu jiulizeni wagombea tulionao wanaweza haya majukumu? Kama wanaweza wape kura, kama unaamini wanaweza majukumu ya kupigania reform (mabadiliko) wape kura, usiwape kwa sababu wamekulaza hoteli fulani,” amesema.

Lissu anayewania uenyekiti katika uchaguzi utakaofanyika Januari 21, 2025 amewataka Bawacha kusimamia msimamo wa kutoshiriki uchaguzi mkuu kama hakutakuwa na mabadiliko yaani no reform no election (hakuna mageuzi hakuna uchaguzi)

Msimamo wa Lissu kwa  Bawacha, ni baraza hilo kutambua viongozi watakaochaguliwa ndio watakaosaidia upatikanaji wa wabunge na madiwani pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Wote mnafahamu wanawake wa Tanzania ni wengi zaidi kwa idadi kuliko wanaume, mnajua wanawake ndio wapiga kura wengi kuliko wanaume na wanawake katika nafasi za uongozi ni wachache kuliko wanaume?

“Inakuaje hawa ambao ni wengi zaidi kwa idadi na wapiga kura wawe wachache zaidi katika uongozi wa bunge na halmashauri?” amehoji.

Lissu amesema ili mwanamke awe mbunge wa viti maalumu ni lazima chama chake walau kipate asilimia tano ya wabunge.

“Kila uchaguzi tunanyang’anywa wabunge sita wa viti maalumu na CCM inapata wabunge hao bure kutokana mfumo, kama mnataka kuongeza idadi ya viti maalumu lazima tuangalie mfumo wa uchaguzi.

“Kama shida ni mfumo wa uchaguzi maana yake tukiwa na mfumo bora wa uchaguzi idadi ya wanawake itaongezeka bungeni, itaongezekaje. Rasimu ya Katiba ya Warioba (Jaji Joseph Warioba) ilipendekeza 50/50 lazima mpiganie mabadiliko,” amesema.

Kauli ya wadau na vyama vya siasa

Awali akitoa ssalamu za, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Taifa Deogratus Mahinjila amesema uchaguzi wa Bawacha ni uchaguzi wa wote.

“Ni uchaguzi wetu sote ombi letu moja mkafanye maamuzi kwa masilahi ya chama, mkachague viongozi wa kuwaunganisha wanawake wote wa Tanzania, mkachague viongozi wa kuwafanya mjisikie mna raha kubwa ya kuwa Chadema,” amesema.   

Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake wa chama cha ACT Wazalendo, Janeth Rithe akitoa salamu zake kwa Bawacha, amesema siasa sio safari fupi kama wengi wao wanavyofikiri, kwani imejaa changamoto ambazo haziwezi kukimbiwa bali kukabiliwa

Amefafanua kuwa changamoto ambayo imejaa katika siasa nchini ni tatizo la usawa wa kijinsia, hivyo jukumu lao ni kuhakikisha wanaleta usawa huo.

“Sisi wanawake tulipata imani kubwa sana hasa ninyi Bawacha baada ya kupata kiongozi mwanamke Tanzania, lakini uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika umetuonyesha dhamira njema haipo,” amesema.

Mkurugenzi wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Bernadetha Kafuko amewataka wanawake wa Bawacha kutumia demokrasia kuwachagua viongozi.

“Ombi langu, sisi tunasimamia demokrasia Tanzania, mkatumie demokrasia ambayo ndio jina la chama chenu kuchagua viongozi, mwenyekiti atakayepatikana atakuwa mwenyekiti wa TCD, baada ya uchaguzi mkawe wamoja”amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Umoja la Wanasiasa na Wanawake (Ulingo), Dk Avemaria Semakafu amesema Bawacha wanapaswa kuhakikisha wanawajenga vijana wadogo wa kike ambao wataongoza nafasi ndani ya Bavicha.

Semakafu amesema wanawake wa Bawacha wamevuka mipaka na kugombea nafasi nyingine akitolea mfano nafasi ya Susan Lyimo aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha).

Related Posts