Dodoma. Wakati maandalizi ya mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), yakipamba moto jijini Dodoma yakiwamo maeneo ya katikati ya jiji kupambwa na bendera za chama hicho, nyumba nyingi za kulala wageni zimejaa kwa siku tatu mfululizo.
Mkutano huo utakaofanyika Januari 18 na 19, 2025 katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Center, utafanya kazi ya kujaza nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama hicho bara.
Nafasi hiyo imekuwa wazi tangu Julai 28, 2024 Abdulrahman Kinana alipojiuzulu.
Leo Alhamisi, Januari 16, 2025, Mwananchi imepita katika baadhi ya nyumba za kulala wageni zilizopo katikati ya jiji la Dodoma na kukuta nyumba nyingi za kulala wageni zimechukuliwa na CCM kuanzia kesho Ijumaa Januari 17,2025 hadi Jumatatu.
“Kama unataka kwa leo utapata lakini kama ni kesho hadi Jumapili huwezi kupata CCM wamechukua vyumba vyote 11. Jaribu katika nyumba nyingine unaweza kupata,” amesema mmoja wa wahudumu wa nyumba ya kulala wageni iliyopo Mji Mpya Dodoma.
Katika nyumba chache za kulala wageni kulikuwa na nafasi lakini wateja walitakiwa kulipia bei ya vyumba hivyo iliyoanzia Sh25,000 hadi 30,000 leo ili kushika nafasi za kulala kesho.
Hali hiyo imekuwa tofauti na mikutano mikuu iliyopita ya chama hicho, watu wengi waliokuwa wakifika Dodoma kwa ajili ya shughuli mbalimbali walikosa sehemu za malazi kutokana CCM kulipia vyumba vyote kwenye hoteli na nyumba za kulala wageni.
Pia, maeneo mbalimbali yamepambwa na bendera za chama hicho, mabango makubwa kwa madogo yanayowakaribisha wajumbe wa mkutano huo jijini Dodoma.
Kwenye ofisi za makao makuu ya CCM, kulikuwa na watu wengi wakitoka na kuingia tofauti na siku nyingine huku nje ya ukumbi huo kukifungwa mahema yaliyowekwa viti.
Aidha, mitaa ya karibu ofisi hizo maarufu White House, baadhi ya wafanyabiashara kutoka mikoa mbalimbali nchini, wamepanga biashara ya sare za chama hicho.
Mfanyabiashara wa maduka ya nguo na hoteli, Peter Olomi amesema wamejiandaa kuhakikisha kunakuwa na huduma bora za hoteli na mavazi zikiwamo sare za chama hicho.
“Chama kinapokuwa na mkutano mkuu kama huu mavazi kama suruali nyeusi, nguo za mama za kijani, suti na kadhalika yanahitajika kwa wajumbe, hivyo tumejiandaa kuwahudumia. Tunajua wanakuja wageni zaidi ya 3,000 kutoka ndani na nje ya nchi ambao wanahitaji huduma zetu katika kipindi hicho,” amesema.
“Kwa upande wa malazi, hali hii imekuwa ikijirudia nyakati zote za mkutano kwa kuwepo kwa mahitaji makubwa, hivyo tumejiandaa kwa kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha katika maeneo tunayotoa huduma, usafi na uwepo wa bidhaa bora na ukarimu,” amesema.
Alipoulizwa kuhusu changamoto ya upungufu wa malazi katika mkutano huo, Olomi amesema vyumba vipo vya kutosha vyenye hadhi zote zinazotakiwa na wajumbe, tofauti na mikutano iliyopita, watu walikuwa wakisumbuka malazi.
“Mikutano iliyopita ilikuwa ni mafunzo kwetu, changamoto zilizojitokeza tulizichukua kama fursa. Sio watu wa Dodoma waliojenga hoteli bali leo hii kuna watu wa Mwanza, Dar es Salaam wamekuja hapa kufungua branch (tawi), niwahakikishie kwa sasa hali ni tofauti sana na tulikotoka,” amesema Olomi.
Mjasiriamali wa sare za CCM, Trabo Bwenda amesema uwepo wa mkutano huo ni fursa ya kujipatia kipato kwa sababu wajumbe wanalazimika kununua sare kabla ya kuingia katika mikutano.
“Hapa tunatoka mikoa tofauti tofauti wapo wa Mwanza, Dar es Salaam, Simiyu, mimi mwenyewe ninatoka Morogoro nimekuja hapa kutafuta fursa ya biashara ya nguo katika mkutano huu,” amesema Mwenda.
Mfanyabiashara wa kuku katika Soko la Majengo, Emmanuel Msangi amesema wanatarajia mzunguko mkubwa wa biashara kutokana na kuongezeka mahitaji ya vyakula kuwa mengi.
“Mkutano wa CCM unakuwa na watu wengi kutoka maeneo mbalimbali, kwa hiyo matarajio yetu, tumaini letu ni kuwa mkutano mkuu wa CCM unakuja na neema kwetu sisi,” amesema Msangi.
Amesema wageni wengi wanaofika Dodoma wamekuwa wakihitaji kula kuku wa kuchoma, hivyo wamejiandaa kuhakikisha kwa kipindi chote wanapatikana ili kukidhi mahitaji hayo.
“Kwa miaka mingi, watu wanapokuja Dodoma wamekuwa wakikimbilia kula kuku wa kuchoma wa kienyeji, hivyo sisi tumejiandaa kuhakikisha sifa hiyo inabakia kwa wageni wetu watakaokuja kwa ajili ya mkutano huu mkuu,” amesema.
Kwa upande wake, mamantilie Husna Hassan amesema wingi wa watu katika mikutano huo, unawawezesha wao kufanya biashara kubwa ukilinganisha na siku nyingine.
“Sio mimi tu mwenye matarajio makubwa ya kupata kipato kikubwa katika siku hizi tatu, bali hata wenzangu wanaochoma kuku, nyama na kuuza vinywaji tunatarajia tutanufaika na mkutano huu kwa kuongeza kipato chetu ingawa ni kwa siku chache,” amesema.
Naye Mkazi wa Dodoma, Dk Damas Mukasa amesema mkutano huo ni fursa kwa wafanyabiashara wote wa Mkoa wa Dodoma na kuhawahamasisha kuchangamkia fursa ya ujio wa mkutano huo.
“Ujio wa mikutano mikubwa kama hii inayofanyika Dodoma ni fursa kubwa kwa wakazi wa mkoa huu kwa kufanya shughuli za biashara mbalimbali. Wajumbe pekee ni zaidi ya 3,000 lakini wana madereva wao wanakula wanalala, hivyo nguo na chakula vitauzika,” amesema.