Mahitaji ya vifaa vya viwandani yaongezeka nchini

Dar es Salaam. Ripoti ya uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa mwaka 2024 inaonyesha uagizaji mkubwa wa vifaa vya viwandani, hali inayoakisi ukuaji wa sekta ya viwanda nchini.

Takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya Sh43.076 trilioni zilitumika kuagiza bidhaa mbalimbali, huku vifaa vya viwandani vikiongoza kwa thamani ya Sh11 trilioni, ikifuatiwa na chuma na bidhaa zake (Sh7.02 trilioni).

Wachumi wameeleza kuwa ongezeko hili linahusiana moja kwa moja na juhudi za Serikali kukuza uchumi wa viwanda kupitia miradi ya maendeleo na sera za uwekezaji.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sekta ya viwanda imekuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya uchumi, hali inayosababisha mahitaji makubwa ya mitambo, mashine na vifaa vingine vya viwandani.

Mhadhiri wa uchumi wa Chuo cha elimu ya biashara (CBE), Dk Dickson Pastory alisema: “Kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa na Serikali, yamevutia wawekezaji kutoka nje, hivyo kuongezeka kwa wawekezaji viwandani kumesababisha kuongezeka kwa uagizaji wa vifaa vya viwandani.”

Alisema miongoni mwa mambo yaliyosisimua sekta ya uzalishaji nchini ni kubadilishwa kwa sera ya uwekezaji ambako kumechangia baadhi ya viwanda kuondolewa kodi na tozo kwa ajili ya kuongeza uwekezaji.

Mchambuzi mwingine wa uchumi, Dk Thobiasi Swai, alisema: “Kwa ujumla inaonekana viwanda vimeongezeka nchini, hivyo kuongezeka kwa uagizaji wa bidhaa ni lazima ili kuwezesha uzalishaji wa bidhaa viwandani.”

Naye mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya, Balozi Morwa alionya juu ya athari zitokanazo na ongezeko hili, akisema kuna haja ya vifaa hivyo kuzalishwa nchini ili kupunguza matumizi makubwa ya fedha za kigeni.

“Kuongezeka kwa uagizaji kunaonesha kuwa hatuna uzalishaji wa vifaa vya viwandani, ni muhimu kufikiria mbinu za kujenga uwezo wa kuzalisha vifaa hivi ndani ya nchi. Hii itasaidia kupunguza matumizi ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa ndani zaidi,” alisema.

Aidha, ongezeko la mahitaji ya vifaa vya viwanda huenda lina uhusiano mkubwa na ongezeko la uwekezaji nchini, kwani, Januari 10, 2024, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri katika kipindi cha Januari hadi Desemba 2024, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili jumla ya miradi 901, ukilinganisha na miradi 526 iliyosajiliwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Teri, miradi hii imeweza kuvutia mtaji wa Sh23.5 trilioni ukilinganisha na mtaji Sh14.44 trilioni iliyotokana na miradi ya uwekezaji kupitia TIC katika kipindi cha Januari hadi Disemba 2023.

Mikoa mitano inayoongoza kwa kusajili miradi ya uwekezaji nchini ni Dar es Salaam (356), Pwani (166), Arusha (64), na Dodoma (47), ambapo asilimia 70.3 (miradi 633) ilisajiliwa katika mikoa hii.

Sekta tano zinazoongoza kwa kusajili miradi mingi ya uwekezaji ni uzalishaji viwandani (miradi 377, 41.8%), usafirishaji (miradi 138, 15.3%), ujenzi wa majengo ya biashara (miradi 91, 10.1%), utalii (miradi 76, 8.4%) na kilimo (66, 7.3%).

Related Posts