Mlalamikaji kesi inayomkabili mwanafunzi IFM aomba kuondoa kesi, Mahakama yaridhia

Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, imeiondoa kesi ya wizi iliyokuwa inamkabili mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) Sadik Mbelwa (20), baada ya mlalamikaji katika kesi hiyo kuiomba mahakama hiyo iifute kesi hiyo.

Mlalamikaji katika kesi hiyo, Joel Mdoe, ameiomba Mahakama hiyo iondoe shauri hilo, muda mfupi kabla ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa.

Mdoe amewasilisha ombi hilo, leo Alhamisi Januari 16, 2025 mbele ya Hakimu Gladness Njau, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.

Bila kutoa sababu, mlalamikaji huyo ameieleza amesema amekwenda  mahakamani hapo kuiomba mahakama hiyo iifute kesi hiyo, ambayo ilikuwa katika hatua za kuanza kusikilizwa baada ya upelelezi kukamilika.

Hakimu Njau baada ya kusikiliza maelezo hayo, amekubaliana na ombi la mlalamikaji huyo na kuiondoa kesi hiyo chini ya Sheria ya Mahakimu Wakazi (MCA).

Amesema kwa kuwa mlalamikaji ameomba kesi hiyo ifutwe, Mahakama haina pingamizi, hivyo ameiondoa chini ya kifungu hicho na mshtakiwa yupo huru.

Kwa mara ya kwanza, mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Januari 10, 2025 na kusomewa shitaka moja la wizi.

Mbelwa alisomewa shitaka lake na karani wa Mahakama hiyo, Aurelia Bahati, mbele ye Hakimu Gladness Njau.

Bahati alidai mshtakiwa huyo anakabiliwa na kesi ya jinai namba 8 ya mwaka 2025.

Karani huyo alidai kuwa mshtakiwa huyo ameshtakiwa chini ya kifungo 258 na 265 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa Desemba 11, 2024 saa 2:45 usiku maeneo ya Kisutu, kata ya Kisutu, kwenye hosteli za Greenlight zinazomilikiwa na Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) aliiba simu moja aina ya Sumsung Galaxy M21 yenye thamani ya Sh520,000.

Pia anadaiwa kuiba Laptop moja aina ya HP yenye thamani ya Sh500,000 vyote vikiwa ni mali ya Joel Mdoe.

Mshtakiwa baada ya kusomewa shitaka lake, alikama kutenda kosa hilo.

Related Posts