Dar es Salaam. Baada ya maswali lukuki kuhusu zilivyotumika fedha zilizokusanywa wakati wa kampeni ya Join the Chain iliyofanywa na Chadema, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika amebainisha kiasi kilichokusanywa na mchanganuo wa matumizi yake.
Kwa mujibu wa Mnyika, kupitia kampeni hiyo Ofisi ya Makao Makuu ya Chadema ilipokea kiasi cha Sh114 milioni kutoka akaunti mbalimbali zilizotumika kuchangisha fedha hizo.
Majibu ya Mnyika yanakuja muda mchache baada ya Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekiel Wenje kusema maswali yote kuhusu fedha hizo aulizwe Godbless Lema.
“Lema alikuwa Mwenyekiti wa Join the Chain leo tunapotaka kujua fedha hizo zilienda wapi maswali yote yaelekezwe kwake,” amesema Wenje leo Alhamisi, Januari 16, 2025 katika mkutano wake na waandishi wa habari.
Maswali kuhusu fedha hizo, yaliwahi kuibuliwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Tundu Lissu aliyesema Katibu Mkuu wa chama hicho ndiye anayepaswa kujibu.
Mnyika amejibu hayo leo Alhamisi, Januari 16, 2025 kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X (zamani Twitter).
Amesema kampeni hiyo ilikuwa maalumu iliyolenga kukusanya fedha kwa ajili ya uendeshaji wa chama hicho kati ya Februari hadi Mei 2022.
“Kwa wakati huo kipaumbele cha kwanza ilikuwa ni kugharamia Mkutano wa Baraza Kuu 2022 ambalo pamoja na agenda nyingine lilisikiliza rufaa za wabunge 19 waliofukuzwa uanachama,” amesema.
Baada ya hapo, amesema fedha za ziada zingetumika kwenye operesheni za chama hicho ikiwemo za madai ya Katiba Mpya.
Katika kampeni hiyo, Mnyika amesema chama hicho kilipokea Sh114 milioni kupitia akaunti ya benki na nambari za simu zilizowekwa wakati huo.
Amesema fedha hizo, ziligharamia sehemu ya gharama za Mkutano wa Baraza Kuu la Chama la Mei 2022.
“Pamoja na fedha taslimu kampeni hiyo iliunganishwa pia na ulipaji wa ada na kadi kidigitali ambapo mapato yote kwa ujumla yalikuwa Sh371 milioni.
“Taarifa ya kiwango cha makusanyo na matumizi ilitolewa kwa Kamati Kuu katika vikao vitatu tofauti kwa nyakati mbalimbali hivyo hakuna mjumbe wa Kamati Kuu anayepaswa kusema hafahamu,” amesema.
Amesema majibu sahihi yanapaswa kuwa ama mjumbe hana mamlaka ya kusemea masuala ya fedha au amesahau takwimu.
“Nimelazimika kuandika kuhusu suala hili kwa kuwa naona limejirudia rudia mitandaoni na kwenye vyombo vya habari lakini mara zote ambazo Katibu Mkuu nimefanya press conferences halijawahi kuulizwa,” amesema.
Ameeleza mahesabu ya mwaka husika wa fedha ikiwemo yaliyohusu mapato na matumizi kutoka kampeni hiyo yalikaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na chama kikapata hati safi.
Baada ya maelezo hayo, Lema aliyekuwa Mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini ambaye kesho Ijumaa ametangaza kuzungumza na waandishi kumjibu Wenje amempongeza Mnyika kwa ufafanuzi huo.
“Ninamshukuru KM (Katibu Mkuu) John Mnyika kwa ufafanuzi huu bora. Nitatoa maamuzi kesho tarehe 17/2/2025 Asubuhi kama nitaendelea na Press Conference,” ameandika Lema akichangia maelezo ya Mnyika.