Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela amesema uadilifu, uwazi na misimamo ya kupinga vitendo vya rushwa ni sababu inayomsukuma kumuunga mkono, Tundu Lissu kuwania uenyekiti wa chama hicho.
Lissu ambaye ni Makamu Mwenyekiti-Bara wa chama hicho ni miongoni mwa wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chadema akichuana na wagombea wengine watatu akiwemo Freeman Mbowe anayetetea nafasi hiyo aliyoiongoza kwa miaka 21.
Uchaguzi huo wa Chadema unaendelea kwa ngazi ya mabaraza na utahitimishwa kwa mkutano mkuu wa uchaguzi utakaofanyika Jumanne ya Januari 21, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Januari 16, 2025 jijini Dar es Salaam, Rhoda amesema kuonyesha msimamo wake hadharani hakulengi kumbagaza Mbowe anayetetea nafasi hiyo, bali anamuheshimu kwa juhudi alizofanya hadi kukifikisha chama kilipo lakini aina ya siasa za sasa bado hazimuhitaji.
Rhoda aliyekuwa mbunge wa viti maalumu wa chama hicho (2015-2020) amesema hayo kipindi ambacho viongozi na wanachama mbalimbali akiwemo aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho, Godbless Lema kumshauri Mbowe kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho kisha amuunge mkono Lissu.
Rhoda amesema pamoja na kwamba ameonyesha msimamo wake lakini hata mahitaji ya wananchi wengi wanamuhitaji Lissu zaidi.
“Wananchi wa Katavi wanamuhitaji Lissu, lakini hata mazingira ya hali ya kisiasa ya nchi yetu yanamuhitaji zaidi yeye ni mtu ambaye akisema jambo anatekeleza, tunajua Mbowe ana busara na hekima nyingi lakini kulingana na siasa za sasa ametufikisha hapa tunaibiwa kura na hakuna msimamo mkali anaoutoa,” amesema.
Amesema kupitia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2025 chama hicho kilipata maumivu makubwa lakini azimio lililotolewa lilikuwa la kawaida, huku akieleza walitarajia wangekuwa barabarani kupinga ushindi wa chama tawala.
“Uchaguzi ule haukuwa wa haki na sasa tunapambana wenyewe ndani lakini adui yetu ambaye alipaswa kukabiliwa ni chama tawala, lakini yote hayo yanasababishwa na hekima nyingi alizonazo Mbowe nao wanatumia mwanya huo kufanya wanayoona kwao ni sahihi,” amesema.
Rhoda amesema aina ya siasa za sasa zinahitajika ngumu na viongozi ambao wakitoa kauli inatekelezwa kwa vitendo na haitakiwi kwenda kufanya mazungumzo mezani kubembelezana.
“Tumeumia kwa muda mrefu lakini hakuna matamko magumu yanayotolewa na chama ya kuonyesha njia kama sehemu ya kukasirishwa na kubinya uhuru wa wananchi kuchagua viongozi, lakini wanakuja kuongozwa na wasiowapenda,” amesema.
Amesema wananchi wengi wanapitia maisha magumu na wamebaki njia panda na hata wakitaka kufanya maandamano hawajitokezi hali inayoonyesha hawakubaliani na mwelekeo wa chama hicho.
“Tunahitaji mtu mwenye dhamira ya kweli kama Lissu ili tuweze kurudisha ari na ushawishi kwa wananchi na tuendeleze mapambano ya kuchukua dola,” amesema Rhoda.
Amesema chama hicho chini ya Lissu na makamu akishinda John Heche uwezo wao wa kupambana na uadilifu wao kitakuwa sehemu salama na kurudisha nguvu zake.
“Katika siasa uadilifu na uaminifu ni mambo muhimu zaidi kuliko vingine kwa mwanasiasa na wananchi wanahitaji kuona mambo ya namna hiyo,” amesema
Rhoda amesema anakubaliana na hoja zote za Lissu ikiwemo ya ukomo wa uongozi ndani ya chama hicho ikiwemo ubunge wa viti maalumu ni muhimu ili kuendelea kutoa fursa kwa wanachama wengine kushiriki siasa.
“Jambo lingine hata hoja ya fedha za ruzuku na matumizi ya fedha yafanyike katika misingi ya haki na uwazi ni mambo yaliyonisukuma kumuunga mkono Lissu, wakuu wa mikoa kichama tunapata shida tumekuwa kama ATM kutoa fedha za kuendesha chama, kila jambo tunatoa fedha zetu mfukoni,” amesema.
Amesema chama hicho kukiwa na uwazi na fedha zikashushwa basi kwenye majimbo kusingekuwa na malalamiko.
“Nafahamu si kwamba chama kina fedha nyingi hata zile za ruzuku lakini ilitakiwa kuwe na uwazi, lakini kuna mambo yanafanyika kwa kificho hali inayoleta shida kwa watu kulalamika,” amesema.