Ramovic kuchukua uamuzi mzito Yanga

YANGA haitaki chochote Jumamosi hii zaidi ya ushindi mbele ya MC Alger. Hali hiyo imemfanya Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Sead Ramovic, kuchukua uamuzi mzito ili kuhakikisha wanatoboa.

Ramovic ambaye leo Januari 16 anatimiza siku 62 tangu atambulishwe kikosini hapo na kuiongoza Yanga kucheza mechi kumi za mashindano tofauti, aamini uwezo wa kuifunga MC Alger upo, hivyo tayari amechora ramani ya kuwamaliza wapinzani wao hao kisha kuweka rekodi ya kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululizo.

Jumamosi wiki hii, Yanga itaikaribisha MC Alger katika mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa Afrika kundi A utakaochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni.

Yanga iliyo nafasi ya tatu katika kundi ikiwa na pointi saba, inahitaji ushindi ili kufikisha pointi 10 zitakazoifanya imalize nafasi ya pili nyuma ya Al Hilal iliyotangulia robo fainali na pointi 10. Kumbuka MC Alger ina pointi nane nafasi ya pili, inahitaji sare pekee dhidi ya Yanga ili kufuzu robo fainali.

Katika mikakati ya kuifunga MC Alger, kuna muunganiko wa vichwa vitatu kutoka benchi la ufundi la Yanga ambavyo vimekuwa na vikao vya muda mrefu kusuka mipango ya ushindi.

Vichwa hivyo vinaongozwa na Ramovic, huku wengine ni Mustafa Kodro na Abdihamid Moallin ambao ni wasaidizi na ukiwakuta mazoezini hata kwenye mechi, wanakuwa karibu muda mwingi wakisuka mipango.

Makocha hao wamefanya kazi ya kuibadilisha Yanga kimbinu na kurudi katika ushindani ikipata matokeo mazuri na kufufua matumaini ya kufuzu robo fainali. Katika mabadiliko hayo, pia kocha wa viungo, Adnan Behlulovic anahitaji sifa zake.

Ramovic na jeshi lake walianza mechi mbili za kwanza hatua ya makundi kwa kupoteza 2-0 dhidi ya Al Hilal nyumbani kisha kupokea kichapo kama hicho ugenini kwa MC Alger.

Matumaini yalirejea baada ya sare ya 1-1 ugenini dhidi ya TP Mazembe, kisha kuichapa timu hiyo nyumbani 3-1. Ikaendeleza wimbi la ushindi ugenini dhidi ya Al Hilal ikiwa ni timu ya kwanza kuwafunga Wasudani hao msimu huu.

Hadi sasa, Yanga chini ya Ramovic ikiwa imecheza mechi 10 za mashindano tofauti, imeshinda saba, sare moja na kupoteza mbili huku ikifunga mabao 23 na kuruhusu manane. Kati ya mechi saba ilizoshinda, sita ni mfululizo jambo linalotoa matumaini ya kuichapa MC Alger, Jumamosi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ramovic alisema kutokana na kusafiri umbali mrefu kutoka Mauritania walikokwenda kucheza na Al Hilal na kushinda 1-0, hawatakuwa na wakati mzuri wa kujiandaa kwa ajili ya mchezo ujao hivyo kazi kubwa itakuwa ni kuwasoma wapinzani kupitia video za mechi zao.

“Tunarudi kwenye uwanja wetu wa nyumbani dhidi ya MC Alger, hatutarajii mchezo rahisi, utakuwa mgumu na wa ushindani, tuna siku chache za kurudisha utimamu baada ya safari ndefu, tunachokifanya ni kuchambua mechi za mpinzani,” alisema kocha huyo.

Ramovic aliongeza kuwa jambo muhimu walilonalo sasa ni kufahamu ubora na mapungufu ya wapinzani wao kabla ya kuwakabili na hawana cha kupoteza kwa sababu wanaamini ndio mchezo wa maamuzi kwao.

“Tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu, hawana timu mbovu, ni bora na washindani, kazi kubwa tunayotakiwa kufanya ni kutumia kila nafasi tutakayotengeneza huku tukijilinda kuhakikisha hatufanyi makosa eneo la ulinzi.

“Hatutaingia na akili ya kutumia uwanja wa nyumbani tukiwa na imani kuwa ni rahisi kwetu kupata matokeo mazuri, kama sisi tumeweza kushinda ugenini na wao pia wana nafasi ya kushinda,” alisema.

Wakati huohuo, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema beki wa kikosi hicho, Yao Kouassi Attohoula ataendelea kuwa nje ya uwanja baada ya kufanyiwa upasuaji huku Maxi Nzegngeli ikielezwa anaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi. “Mchezaji wetu Yao hatakuwa sehemu ya kikosi baada ya kufanyiwa upasuaji. Yao atakuwa nje kwa kipindi kisichopungua wiki nne na kisichozidi wiki sita. Maxi anaendelea vizuri na maozezi, kama mwalimu ataona utimamu wake wa kimwili unafaa kucheza mchezo ujao basi atamtumia lakini kimsingi kwa sasa yupo salama.”

Wapinzani wa Yanga, MC Alger kupitia kocha mkuu, Khalid Bin Yahia walisema wanafahamu ugumu watakaokutana nao mbele ya Yanga kwani ni timu yenye wachezaji wapambanaji huku akibainisha kuwa watawakosa wachezaji wawili.

“Hapa Algeria hakuna asiyeifahamu Yanga, huo ndio ukweli, ni klabu yenye wachezaji wapambanaji na imara kimwili dakika zote 90, wachezaji wetu wanajua ugumu wataokutana nao Tanzania lakini jambo jema kwetu ni kwamba hata sare inatosha kutupeleka hatua ijayo ya robo fainali.

“Tunaelekea Tanzania bila ya kiungo Mohamed Zougrana na Beki Merwane Khelif, hao pekee ndio tutawakosa na athari yao ya kukosekana katika kikosi changu siwezi sema ni kubwa sana kwani nafasi zao zina watu wenye viwango sawa na vyao,” alisema.

Related Posts