DROO ya mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (Chan) 2024, itakayofanyia Agosti mwaka huu, imefanyika juzi huku Tanzania ikiangukia kundi ‘B’ na timu za Mauritania, Madagascar, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Katika droo hiyo iliyochezeshwa juzi katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta Kenya, ‘Kenyatta International Convention Centre’ (KICC), itashuhudia nchi tatu zikiandaa michuano hiyo ya nane ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Mwanaspoti linakuletea uchambuzi wa kundi ‘B’ linaloundwa na timu mwenyeji Tanzania, Mauritania, Madagascar, Burkina Faso na Jamhuri ya Afrika ya Kati, ambalo linaonekana sio gumu na kutoa matumaini makubwa kwa Watanzania kufanya vizuri.
Fainali za mwaka huu zitakuwa ni za tatu kwa Tanzania kushiriki baada ya kufanya hivyo mwaka 2009 ilipoangukia kundi ‘A’ na kuishia makundi, ikimaliza nafasi ya tatu na pointi nne, nyuma ya Zambia na Senegal zilizomaliza na pointi tano kila moja.
Katika kundi hilo Ivory Coast iliburuza mkiani na pointi moja, huku Tanzania ikishiriki tena mwaka 2020 na kuishia tena makundi, ilipomaliza nafasi ya tatu kundi ‘D’ na pointi nne nyuma ya Guinea na Zambia zilizomaliza na pointi tano kila moja.
Fainali hizo, Tanzania ilianza kwa kupoteza dhidi ya Zambia kwa mabao 2-0, kisha ikaifunga Namibia bao 1-0 na mechi ya mwisho ikatoka sare ya mabao 2-2 na Guinea, huku Namibia ndio iliyoburuza mkiani baada ya kukusanya pointi yake moja tu.
Mafanikio makubwa kwa Mauritania ni kufika hatua ya robo fainali ya michuano hii mwaka 2022 ambapo ilishindwa kuwika na kutolewa kwa kufungwa bao 1-0, dhidi ya Senegal, mchezo uliopigwa Uwanja wa 19 May 1956 Annaba huko Algeria Januari 27, 2023.
Katika mwaka huo, Mauritania iliongoza kundi ‘D’ na pointi zake nne baada ya kushinda mchezo mmoja na kutoka sare mmoja pia, huku Angola ikiwa na pointi mbili, wakati Mali iliburuza mkiani na pointi moja, kufuatia kila timu kucheza michezo miwili.
Timu hii imeshiriki CHAN mara tatu ambapo zote imeishia hatua ya makundi ikianzia mwaka 2014 ilipoangukia kundi ‘B’ na kumaliza mkiani na pointi moja, nyuma ya Morocco na Zimbabwe zenye tano kila mmoja, huku Uganda ikiishia na pointi nne.
Mwaka 2018, ikashiri tena na kupangwa kundi ‘D’ na kumaliza nafasi ya tatu na pointi mbili, nyuma ya Congo iliyomaliza kinara na pointi saba, ikifuatiwa na Angola iliyokuwa na pointi tano, huku Cameroon ikiburuza mkiani na pointi moja tu.
Baada ya hapo ikashiriki tena fainali zilizofanyika Cameroon mwaka 2020 na kumaliza nafasi ya tatu kundi ‘A’ na pointi nne, nyuma ya Mali iliyokuwa na saba, Camaroon ikimaliza ya pili na pointi zake tano, huku Zimbabwe ikiwa haina pointi.
JAMHURI YA AFRIKA YA KATI
Hii ndio timu inayoonekana ya kinyonge kwa sababu inashiriki michuano hii kwa mara ya kwanza katika historia yake ingawa haiwezi kuchukuliwa poa, kwani inaweza kuwashangaza wengi kutokana na kutopewa uzito kama nyingine zilizowahi kushiriki.
Kundi linalooneka ni la kifo ni ‘A’ ambalo waandaaji wenza Kenya watakumbana na timu za Morocco, Angola, DR Congo na Zambia.
Kundi lingine mbali na ‘B’ ambalo ni la Tanzania, lipo la ‘C’ lenye timu za Uganda ambao ni waandaaji wenza pia kama ilivyokuwa kwa Tanzania na Kenya ambao wamepangwa na Niger, Guinea huku timu zingine tatu zikisubiriwa ambazo zitafuzu.
Kundi ‘D’ lina timu za Senegal ambao ndio bingwa mtetezi wa michuano hiyo akipangwa na Congo, Sudan, Nigeria ambapo kwa mwaka huu mashindano hayo yanafanyika Afrika Mashariki kwa mara ya kwanza tangu mara ya mwisho Rwanda ilipoandaa 2016.