Mwenyekiti wa Kamati ya michuano ya Jafo Cup Ally Mkomwa akikabidhi mpira na jezi na Kocha wa timu wa Kisarawe Muada Semkiwa Mhando kwenye hafla iliyofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Kisarawe Mkoani Pwani leo Januari 16.
Afisa Michezo Wilaya ya Kisarawe Dalidali Rashid
Na Khadija Kalili Michuzi TvTIMU nne zinatarajiwa kushuka dimbani mwishoni mwa wiki ikiwa ni katika mzunguko wa nusu fainali ya michuani inayoendelea ya ‘Jafo Cup’ Wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani
Akizungumza na Waandishi wa Habari kwenye mkutano uliofanyika leo tarehe 16Januari, 2025 Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi Ally Mkomwa amezitaja timu hizo kuwa ni Kisarawe , Marui, Manerumango na .
“Michuano ya Jafo Cup imeanza mwaka jana 2024 na imeshirikisha timu kutoka kata zote 17, vijiji 65 na Vitongoji 232 huku lengo kuu la michuano hii ni kuvumbua vipaji vya vijana na kuviendeleza kwa ujumla” amesema Mkomwa.
Mkomwa amesisitiza kuwa mbali ya kukuza vipaji pia ni moja ya mchakato wa kuunda kikosi cha timu itakayokuwa na jina la Mheshimiwa Jafo ambaye pia ndiyo Mbunge wa Jimbo hilo pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara.
“Nusu fainali hizo zitachezwa katika mtindo wa mechi ya nyumbani na ugenini huku Januari 18 timu ya Kisarawe itasguka dimbani kukipiga na Kurui kwenye Uwanja wa Manerumango na Januari 18 siku ya Jumapili timu ya Manerumango itacheza na Marui kwenye Uwanja wa Chole” amesema Mkomwa.
Amezitaja zawadi wa washindi waliofuzu kuingia nusu fainali kila timu itapewa kitita cha 300,000 na jezi huku kwenye fainali mshindi ataondoka na done nono kiasi cha Mil.2 pamoja na pikipiki mbili huku mshindi wa pili ataondoka na Mil.1 pamoja na pikipiki moja huku timu zitakazoshika nafasi ya nne na ya tano wapewa mipira.
Wakati huohuo Afisa Michezo Wilaya ya Kisarawe Dalidali Rashid ametoa shukrani za dhati kwa Mhe. Mbunge wa Kisarawe Selemani Jafo kwa moyo wake na jinsi anavyojitoa katika kusaidia michezo kwenye ngazi mbalimbali Jimboni kwake sambamba na kutoa hamasa ya wapenda michezo wote nchini kujitokeza kwa wingi siku ya fainali ya Jafo Cup itakayochezwa Manerumango Februari 2 mwaka huu Wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani.
Mhe.Jafo ni Mjumbe wa Bodi Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoani Pwani .