Vurugu zazuka nje ya ukumbi wa uchaguzi Bawacha

Dar es Salaam. Katika hali isiyokuwa ya kawaida, ugomvi wa ngumi umezuka nje ya Ukumbi wa Ubungo Plaza unapofanyika mkutano wa uchaguzi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha).

Ugomvi huo ulikuwa kati ya wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu dhidi ya wafuasi wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Ingawa mkutano huo wa uchaguzi ulioanza mchana wa jana Alhamisi, Januari 16, 2025 unaofanyika ni wa wanawake, lakini waliorushiana ngumi walikuwa wanaume.

Chimbuko la ugomvi huo ni mabishano ya kuimarishwa kwa ulinzi, yaliyosababisha kutiliwa shaka mmoja wa watu waliokuwepo katika lango kuu la Ukumbi wa Ubungo Plaza.

Mabishano hayo, yalisababisha walinzi kuanza kumuondoa mtu huyo na wengine waliokuwepo eneo hilo na kuanzia hapo watu walianza kushambuliana.

Ugomvi ulidumu kwa takriban dakika 15, muda mfupi baadaye gari aina ya Prado lililodaiwa kubeba baadhi ya watu waliokuwa sehemu ya ugomvi huo liliondoka kwa kasi kuelekea Manzese.

Hata hivyo, Mwananchi iliarifiwa kuwa, baadhi ya walinzi wanaodaiwa kumuunga mkono Lissu, walinyimwa vitambulisho vya kuifanya kazi hiyo katika ukumbi huo, hivyo hawakutakiwa kuonekana.

Baada ya ugomvi huo wa ngumi, baadhi ya waliokuwepo eneo hilo walitupiana lawama wakisema inawezekanaje waalikwe watu wa kupigania wenyewe kwa wenyewe.

“Inakuwaje mwana Chadema unaalika watu wa kumpiga mwana-Chadema mwenzake, wakati huu ni uchaguzi,” amesikika mmoja wa mashuhuda aliyekuwa amevalia gauni lenye nembo ya Bawacha.

Baada ya kukamilika kwa uhakiki wa wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), hatimaye muda wa kuanza kusikiliza sera za wagombea umewadia.

Wito wa kuwataka wajumbe kurudi ndani ya ukumbi, umetolewa saa 5:30 usiku, sambamba na wagombea wa nafasi zote.

Sababu ya wito huo ni kutoa nafasi kwa wagombea wa nafasi ya ujumbe wa baraza kuu la chama hicho, waanze kunadi sera zao kisha wapigiwe kura.

Nafasi hiyo pekee ina jumla ya wagombea 24 kutoka Bara na watatu kwa upande wa Zanzibar.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa mbalimbali

Related Posts