KENGOLD wameshtuka. Baada ya kupima upepo wa Ligi Kuu Bara na kubaini sio mwepesi, mabosi wa klabu hiyo iliyopanda daraja msimu huu wameamua kufanya kweli kwa kushusha majembe ya maana yanayoweza kushtua katika duru la pili, licha ya kuwakosa Saido Ntibazonkiza, Luis Miquissone na Tadeo Lwanga.
Kikosi hicho cha Wachimba Dhahabu wa Chunya, kimewakosa nyota hao wa zamani waliowahi kutamba na Simba katika dakika za lala salama kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili kutokana na masilahi, lakini bado kuna vifaa vingine 24 vimeanza kukiwasha mazoezini.
Mwanaspoti lililotimba katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Isyesye jana asubuhi, liliwashuhudia wachezaji wapya na wale wa zamani wa timu hiyo akiwamo Bernard Morrison ‘BM3’, ambaye hata hivyo hakushiriki kwani aliishia nje.
Kinachoshtua ni kwamba mastaa hao wapya waliosajiliwa na timu hiyo baadhi yao ni wakongwe na wazoefu waliowahi kucheza Ligi Kuu kupitia klabu kubwa za Simba, Yanga na Azam FC, kitu kinachofanya mashabiki wa soka kutaka kuona wanatokaje katika lala salama ya Ligi Kuu.
Msimu uliopita Mashujaa iliyokuwa imepanda Ligi Kuu ilianza vibaya na kuonekana kama ingeshuka daraja kabla ya kutumia dirisha dogo kama hili kusajili majembe ya maana na kupambana na mwishowa msimu ilimaliza katika nafasi ya nne na kuepuka na janga la kushuka lililoondoka na Mtibwa Sugar na Geita Gold zinazochuana kwa sasa katika Ligi ya Championship zikifukuzana kileleni kutaka kurejea Ligi Kuu.
KenGold inayoburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu msimu huu ikivuna pointi sita tu kutokana na mechi 16 ilizocheza hadi sasa, ni kama imeamua kuamka usingizi ili kuepuka kushuka daraja kwa kusajili mashine 24 mpya na kuacha 11.
Pia ipo mbioni kumtambulisha kocha mpya, Vladslav Heric raia wa Serbia aliyekuwa akiinoa Venda FC ya Afrika Kusini mbali kupita pia klabu nyingine kama Chippa Utd, Cape Town na Free State Stars. Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo wamesema wameamua kushusha mashine hizo wakiwamo nyota wa kigeni kwa lengo la kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika duru la kwanza kwa kupata ushindi wa mechi moja na sare tatu, huku wakipoteza mechi 12 na anaamini kila kitu kitakaa sawa mechi zijazo.
Licha ya kigogo huyo kutoweka bayana ishu ya kocha Heric, lakini Mwanaspoti linafahamu yupo jijini Mbeya na wameshamalizana naye kila kitu. Mbali na Morrison aliyewahi kuwika Simba, Yanga na Far Rabat ya Morocco na Chirwa aliyekipiga Yanga na Azam kabla ya kuibukia Namungo na Kagera Sugar.
Pia KenGold imenasa wakali wengine kama Zawadi Mauya aliyewahi kutamba na Kagera na Yanga, Emmanuel Asante (Namungo), Mubashid Seidu (Ghana), Kyala Lassa (Zambia), Elnest Kwofie (Ghana), Kelvin Yondani, Mohamed Yusuph (Dodoma Jiji), Mathias Juviliani, Nassir Bofu, Abdul Abdulai, Thompson Unachi (Nigeria), Maulid Mbegu, Sele Bwenzi, Joseph Ambokege, Ahmed Chambela, Sadala Lipangile, Sandale Komanje, Rojas Gabriel, Fredrick Kalubunga (Vipers) na Erick Kabamba.