Waliovamia hifadhi ya Iluma kuondoka kwa hiari

Ulanga. Mkuu wa wilaya ya Ulanga, Dk Julius Ningu amesema hatua ya  kuwaondoa wananchi waliovamia eneo la hifadhi ya jamii ya Iluma iliyopo kijiji cha Mbuyuni kata ya Minepa wilayani humo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa bila ya kutumia nguvu kubwa ya vyombo vya dola.

Akizungumza na Mwananchi, Dk Ningu amesema kabla ya kutoa agizo la kuondoka katika hifadhi hiyo alipata fursa ya kuzungumza na wananchi hao kuwataka waende wakatafute makazi kwenye vijiji vingine vilivyopo kwenye wilaya hiyo na hata nje ya wilaya hiyo.

“Hawa wananchi hawakuwa na nyumba za kudumu bali walikuwa na vibanda vilivyojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi, hivyo siku tatu nilizotoa nilijua zinatosha kabisa kuwafanya wananchi hawa kuondoa vitu vyao ikiwemo miti waliyojengea hizo nyumba,” amesema Dk Ningu.

Amesema wananchi hao wako huru kwenda kokote na tayari ameshawasiliana na wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata kuwapokea na kuwapa maeneo halali ya kuishi, hivyo amewataka wananchi hao kufuata sheria na kanuni za kuomba maeneo kwa ajili ya makazi.

 Ngunda Nangi ni mmoja wa wananchi wanaodaiwa kuvamia hifadhi hiyo na baba mwenye watoto saba ambapo kwa sasa amelazimika kuondoka kutokana na agizo hilo.

Amesema kwa vile agizo la kuhama limetolewa na Serikali hawezi kukaidi japokuwa limeacha machungu na hasara kubwa hasa baada ya kukosa makazi na hivyo kujikuta akiishi chini ya miti na familia yake.

“Kuna watoto wangu wanne wanaosoma wakiwemo wa shule ya msingi na sekondari na mpaka sasa sijui watasoma wapi kwa kuwa sijui naenda kuishi wapi,” amesema Nangi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbuyuni, Raphael Makindamba amesema zaidi ya kaya 50 zilikuwa zimevamia hifadhi hiyo ambapo mpaka kufikia leo karibu kaya zote zimeshaondoka katika hifadhi hiyo.

Related Posts