Arusha. Zaidi ya wanafunzi 150 wa jamii ya wafugaji wa Kimasai waishio Kijiji cha Kimokouwa, wilayani Longido, Mkoa wa Arusha wamepatiwa misaada ya vifaa mbalimbali vya shule.
Misaada hiyo imetolewa hivi karibuni na Shirika la ‘Smile Youth and women Support Organisation’ la jijini Arusha, kwa lengo ni kusaidia wanafunzi hao wa shule za msingi na sekondari kupata mahitaji yao muhimu ikiwemo sare na madaftari.
Akizungumza baada ya kupokea misaada hiyo, mmoja wa wanafunzi hao, Musa Melita amewashukuru wadau hao kwa msaada huo ambao utawawezesha wakiwa na mahitaji yote muhimu kama wanafunzi wengine.
“Tulikuwa na changamoto ya kwenda shule kwa wakati kwa sababu tulikuwa hatuna sare wala mahitaji mengine muhimu kama madaftari, ila kwa sasa tunashukuru msaada huu utatuwezesha kwenda shule kwa wakati na tutasoma kwa bidii,” amesema Melita.
Naye Losinyati Laizer ambaye ni mmoja wa wazazi wa watoto walionufaika na msaada huo, amesema hiyo inawapa ari kama wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.
“Ilikuwa ni ngumu kupata fedha kwa ajili ya kurudisha watoto shule ila tunashukuru wadau kwa kutusaidia, tunazidi kujifunza umuhimu wa kupeleka watoto shule na kuwapatia mahitaji ya muhimu ya kila siku.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Kimokouwa, Sarone Olekuku amesema wanaendelea kupambana kupunguza utoro shule kwa kisingizio cha kukosa mahitaji muhimu ya shule ikiwemo madaftari.
Awali, Mkurugenzi wa shirika hilo, Omega Mlay amesema kuwa lengo la misaada hiyo ni kuhakikisha wanafunzi hao wa pembezoni wanapata haki yao ya msingi ya kusoma kama wanavyopata wengine.
“Serikali inatoa elimu bure na sisi kama wadau tunajitahidi kushirikiana kuiunga mkono kwa kupatia watoto mahitaji muhimu ya shule ili waweze kuhudhuria masomo kwa wakati na kuepusha visingizio vya ukosefu wa vifaa vya kujifunzia, kwani tunatamani jamii hizi zipate elimu,” amesema.
Mratibu wa shughuli hiyo, Elia Mushi amesema jamii za pembezoni zimekuwa zikisahaulika na misaada mingi huishia mijini ndiyo maana wao wamejikita kuhakikisha wanatembelea na kusaidia jamii hizo za pembezoni zenye uhitaji.
Baadhi ya misaada iliyokabidhiwa kwa wanafunzi hao ni daftari, kalamu, sare za shule na mafuta ya kujipaka.