Wananchi Ubungo walilia barabara | Mwananchi

Dar es Salaam. Baadhi ya wananchi wa Mpigi Magohe, Wilaya ya Ubungo wameikumbusha Serikali kutekeleza ahadi ya ujenzi wa barabara ya Mbezi Victoria kwa kiwango cha lami iliyotoa ili kuwaondolea adha ya usafiri inayowasumbua.

Ahadi ya ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 9.55 yenye kero hususan nyakati za mvua ilitolewa Mei 2024 na aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ambaye kwa sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Januari 16, 2025, Mbunge wa Kibamba (CCM), Issa Mtemvu amesema hata yeye yupo njia panda hajui kinachoendelea na anakosa majibu ya kuwaeleza wananchi wake kwani si barabara hiyo tu, barabara nyingi ambazo makandarasi walikuwa kwenye ujenzi wamesimama.

“Si barabara ya Victoria pekee lakini kuna barabara zingine mikataba imeshasainiwa na makandarasi walianza kuingia eneo la kazi,’’ amesema.

Mtevu amesema barabara ya Matosa hadi Kimara Temboni zimesimama na nyingine nyingi lakini majibu ni mtambuka ambayo kama mbunge amekosa majibu lakini Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) wanaweza kuwa na majibu sahihi.

Wananchi hao wamedai Bashungwa alitoa ahadi hiyo baada ya kuwatembelea kusikiliza kilio chao cha kusumbuliwa na barabara hiyo na aliwaahidi ingeenza kujengwa kuanzia kuanzia Novemba 2024 kwa kiwango cha lami lakini hakuna kinachoendelea.

Alipotafutwa na Mwananchi, Meneja wa Tanroads, Mkoa wa Dar es Salaam, John Mkumbo amesema mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo bado upo kwenye hatua za ununuzi.

“Taratibu za kiununuzi zikikamilika na taratibu zingine zitafuata kwa sababu hatua za ununuzi kwa kuanza tumetangaza kilomita 12 baada ya kupata bajeti ya mwaka huu,” amesema Mkumbo

Amesema barabara hiyo ni kubwa na imezunguka kutoka Mbezi Magufuli hadi Bunju ni wastani wa kilamita 23 na kuna baadhi ya vipande vingine kwenda Mpigi Magohe vimekamilika na vingine vitakamilishwa.

Wakizungumza wakazi hao hivi karibuni wakiwa kwenye mkutano wa kujadili changamoto zinazowakabili, walidai kwa sasa barabara inawaumiza zaidi ina mashimo mengi huku wakieleza hata gharama za maisha zinapanda zaidi mvua zikianza.

“Waziri Bashungwa alituahidi hadi Novemba mwaka jana ingeanza kujengwa kwa kuona magreda kuzunguka lakini tunashangaa kimya na imekuwa ajenda ya kutengenezwa kwa muda mrefu,” amesema Fredy Lyimo

Amesema kwakuwa Serikali ilishatoa ahadi hiyo ya kutengeneza kwa muda mrefu na mwaka uliopita Waziri Bashungwa alikuja kuzungumza maeneo hayo hadharani ni muhimu mipango hiyo iharakishwe ili wananchi wapate ahueni.

“Hata kwa waziri aliyepo sasa (Abdallah Ulega) anapaswa kujua mtangulizi wake alikuja kutoa ahadi ya kutujengea barabara lakini hadi sasa hatuoni kinachoendelea inakuwaje tunatambua nyaraka zipo,” alisema.

Mkazi wa Msakuzi, Philbert Mosha ambaye ni mratibu wa kikundi cha wanaume cha Msakuzi Neighbour amesema barabara ni changamoto inayowasumbua kwa muda mrefu sasa.

“Kipindi cha masika hali kwetu inakuwa ngumu zaidi kuna wanakosa usafiri kwakuwa barabara mbovu hazipitiki, na hata wachache wanaojitosa kuleta usafiri wao gharama zinakuwa kubwa kiasi kwamba walio wengi wanashindwa kumudu,” amesema.

Related Posts