Wananchi wazua vurugu msibani, waking’ang’ania kumzika mwenzao

Arusha. Vurugu zimeibuka katika Mtaa wa Ilkirouwa, Kata ya Lemara jijini Arusha baada ya wananchi wa eneo hilo kuweka kambi katika nyumba ya familia ya Bariki Tarimo (41) aliyefariki dunia, wakishinikiza kijana huyo azikwe katika eneo hilo alilokuwa akiishi na mama yake mzazi ambaye alishafariki dunia na sasa anaishi mama yake wa kambo anayetajwa kuwa ni raia wa nje na hata jina lake halifahamiki.

Hata hivyo, Mwananchi lilipotaka kujua wapi alipo baba yake Bariki, majirani pia wamesema haishi hapo na hawajamuona kwa muda mrefu.

Inadaiwa baada ya taarifa za Bariki kuwa amefariki dunia, baadhi ya ndugu zake wamejitokeza na kutaka kuchukua maiti yake na kwenda kuizika Njiro huku wakisema hakuna msiba unaoendelea hapo nyumbani kwao.

Hivyo, wananchi na majirani ndipo wakazua  vurugu hizo jana wakishinikizwa mwili wa Bariki uzikwe katika eneo hilo na badala ya kwenda kuzikwa makaburi ya Njiro, Arusha.

Akizungumza jana Jumatano Januari 15, 2025 katika msiba huo, Balozi wa nyumba kumi katika mtaa huo, Rebeca Obeid alisema Bariki aliugua kwa muda mrefu bila msaada wa ndugu zake na alikuwa akilala kwenye chumba cha mfanyakazi kilichopo karibu na mabanda ya mifugo na baadhi ya wakazi wa eneo hilo walikuwa wakimchangia fedha za matibabu na chakula.

Amesema kijana huyo ameugua kwa muda mrefu lakini ndugu zake walimtenga, hali iliyoulazimu uongozi wa eneo hilo na wananchi kuchangishana fedha kwa ajili ya kuhakikisha Bariki anapata matibabu na chakula.

Na Jumatatu Januari 13,2025 usiku Bariki alifariki dunia akipatiwa matibabu Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Alhamisi Januari 16, 2025 Balozi Obeid amesema; “Wananchi wana hasira na uchungu kwa sababu wakati anaumwa, familia ilikuwa imemtenga, baada ya kumtenga serikali ya mtaa na wananchi wakachukua jukumu la kupita nyumba hadi nyumba kuchangisha fedha ili kumsaidia apate matibabu na chakula,” amesimulia Obeid.

Amesema ilifikia hatua yeye na wajumbe wenzake walishawahi kufika kwa ndugu zake kuwaelezea hali aliyokuwa akiipitia Bariki, lakini hawakushtuka.

“Tumepiga simu hadi Dar es Salaam kwa baadhi ya ndugu zake, hatukupata ushirikiano,” amesema mjumbe huyo.

Akizungumza na Mwananchi, mjomba wa marehemu Bariki, John Meresho anayeishi Dar es Salaam, amesema alipata taarifa za kifo cha Bariki kupitia mitandao ya kijamii.

Amedai hakuwa na taarifa za ugonjwa wake. “Nilipokuwa nikiperuzi simu yangu, nikaona taarifa za Bariki. Nilimpigia simu kaka yake ambaye naye anaishi Dar es Salaam, naye akaniambia ameona video inayozungumzia habari za mdogo wake. Nikamuuliza kama ana uhakika ni yeye, ana mpango wowote wa kwenda Arusha lakini mimi nilianza safari mara moja kuja Arusha.”

Hata hivyo amesema alienda moja kwa moja Arusha kabla ya kuwajulisha ndugu wengine kwa lengo la kuthibitisha kama kweli kijana wao amefariki dunia.

“Kwa kweli nimefika na nimesikitishwa sana na mazingira ya kifo hiki. Ninachokisikia hapa ni ukweli. Bariki ana ndugu (upande wa baba) wenye uwezo mkubwa, hata mimi wangeniambia kama anaumwa, ningekuja kumsaidia lakini hawakuniambia,” amesema mjomba huyo.

Kuhusiana na nyumba, Meresho amesema Bariki alipatiwa nyumba  na marehemu mama yake pale eneo la Sakina.

Hata hivyo, anasema mama huyo alipofariki dunia, mumewe hakushiriki mazishi.

“Hata msiba wa dada yangu (mama wa Bariki) ulikuwa na changamoto kama hizi. Baba wa Bariki alikataa kumzika dada yangu ila alisema  apelekwe Marangu ndiko tulikomzika,” amesema Meresho.

Aliyekuwa mke wa Bariki, Mary Kaaya naye amesema walitengana na mumewe si kwa sababu waligombana, bali kutokana na changamoto za kifamilia upande wa mumewe. Amesema Bariki alichukua jukumu la kumuuguza baba yake, na hali hiyo ilisababisha mabadiliko katika ndoa yao.

“Nilikuwa mke wa Bariki, na hatukutengana kwa ugomvi. Tulitengana kwa sababu Bariki alitaka kubaki nyumbani ili kumuuguza baba yake tangu mwaka 2012.

“Tulipooana tulikuwa tunaishi kwenye nyumba ya kupanga, lakini baba yake alipoanza kuumwa, tukarudi hapa nyumbani lakini hali haikuwa nzuri, mimi nikaamua kuondoka zangu, mpaka leo huyo baba ni mgonjwa,” amesema.

Naye Joseph Kimaso, mkazi wa eneo hilo amedai kuwa Bariki amezaliwa katika eneo hilo, lakini  ndugu hawataki kumzika katika eneo hilo na kudai chanzo ni marehemu kutajwa alikuwa mtoto wa nje ya ndoa.

“Bariki ana mtoto mmoja ila haishi hapa, ndugu zake hawataki kumzika hapa ili mtoto asije kupata urithi wa eneo hili, sisi tunataka msiba uwepo hapa na tuweze kumsitiri ndugu yetu kwa heshima,” amesema Kimaso.

Naye Sebastian Msaki amesema licha ya familia kutokuweka msiba nyumbani hapo, wananchi wameamua kuchangishana fedha na wanaendelea maombolezo nje ya nyumba hiyo.

“Bariki tulikuwa tunaishi naye vizuri ni mtu wa watu, jana tumekata ndizi mgombani tumepika hazina nyama lakini tulipika ili tuomboleze, tunajichanga tuendelee na maombolezo. Mimi ni mpishi na nimejitolea nitapika na kupamba bure,” amesema Msaki.

Jirani mwingine, Upendo Joel amesema, “sisi shida yetu watukubalie msiba uwepo hapa na shughuli zote zifanyike hapa halafu wao kama familia, waamue wanaenda kuzika wapi tusingekuwa na kelele, tulipokuja walisema hamna msiba kivipi yaani, yaani tuishi naye, tumuuguze atufie halafu wanakuja kutudharau wanasema hapa hakuna msiba hii haiwezekani.”

 “Tumempeleka Bariki hospitali hajapata huduma ya ndugu yeyote, eti amekufa leo ndiyo ndugu wenye fedha wanajitokeza wanataka Bariki wakamzike sijui wapi, tumeambiwa hapa hamna msiba kuanzia mwanzo, hii siyo sawa,” amesema Joel.

Jana mwakilishi wa ukoo, ambaye alitajwa kwa jina la Michael Tarimo  aliingia kwenye matatizo baada ya kushindwa kutoa majibu kuhusu hatima ya maziko ya kijana huyo na aliokolewa na baadhi ya viongozi na Polisi waliofika msibani hapo.

Akizungumza na wananchi hao, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Albert Kilembu amesema wameshafanya mazungumzo na familia na kuwaomba wananchi hao kusubiri uamuzi utakaotolewa na familia baada ya vikao vyao.

Baada ya kikao baina ya familia ya Bariki,  uongozi wa mtaa na diwani wa Lemara kilichofanyika leo, imekubaliwa maziko ya kijana huyo yatafanyika kesho, Ijumaa Januari 17, 2025, katika eneo la Sakina, jijini Arusha.

Related Posts