Unguja. Wafanyakazi wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA), wametakiwa kusimamia manunuzi kwa mfumo wa mtandao kwa lengo la kuboresha ufanisi wa kazi na kuondoa makosa upotevu wa mapato.
Hayo yamesemwa leo Januari 16,2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo Mtumwa Said Sandali wakati akifungua mafunzo kwa bodi ya manunuzi wa ZMA mjini Unguja.
Amesema, watendaji wanaosimamia bodi ya manunuzi wanapaswa kufanya kazi zao kwa kutumia mfumo wa ununuzi mtandao (EPROZ) badala ya kutumia utaratibu wa zamani. Amefafanua kuwa mafunzo hayo yatawasaidia washiriki hao kutekeleza majukumu yao kwa usahihi na weledi, hivyo amewataka kuyapokea vyema na kuyafanyia kazi ipasavyo.
“Ripoti nyingi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Hesabu za Serikali (CAG) huko nyuma zilikuwa zikiwasisitiza watendaji wa Serikali na bodi za manunuzi kuzingatia utaratibu wa kufanya manunuzi kwa kutumia mfumo wa EPROZ kwa lengo la kuondosha upotevu wa mapato,” amesema Mtumwa
Naye, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi, Ali Said Ali amesema lengo la mafunzo hayo ni kuimarisha kitengo cha manunuzi ili kuhakikisha wanatekeleza majukumu yaliyoainishwa katika sheria ya manunuzi.
Pia, amesema mafunzo hayo yatawajengea uwezo wajumbe wa bodi ya zabuni juu ya utaratibu wa sheria na kanuni katika kutekeleza majukumu yao kupitia mfumo wa EPROZ.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa ZMA, Harrieth Lyimo amesema mafunzo hayo yataifanya bodi ya uzabuni kuboresha kazi na kuonyesha makosa yapo wapi ili kuyaepuka.