Watatu kortini kwa tuhuma za uzembe, uzururaji Dar

Dar es Salaam. Wakazi watatu wa jijini hapa, wamefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kujibu shitaka la uzembe na uzururaji.

Washtakiwa hao ni Juma Khamisi (20), Abubakari Gidamanonga (32) na Kaiza Tibangayuka (38).

Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi Januari 16, 2025 na kusomewa shitaka lao na karani Aurelia Bahati, mbele ya Hakimu Gladness Njau.

Akisoma shitaka hilo, Karani Bahati, amedai washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Januari 14, 2025, katika barabara ya Barack Obama, iliyopo wilaya ya Ilala.

Inadaiwa washtakiwa hao walikutwa wakiwa wanazurura mitaani bila kazi ya kuwaingizia kipato, huku wakijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Washtakiwa baada ya kusomewa shitaka hilo walikana na upelelezi  wa shauri umekamilika.

Hakimu Gladness, alitaja masharti ya dhamana kuwa kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho watakao saini hati ya dhamana ya Sh100,000 kila mmoja.

Hata hivyo, washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Hakimu Njau aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 28, 2025.

Related Posts