Watatu mbaroni tuhuma za kuwauzia wakulima mbegu feki

Njombe. Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa kushirikiana na Taasisi ya Kudhibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI), limefanikiwa kuwakamata watu watatu wanaotuhumiwa kuwauzia mbegu feki wananchi katika kijiji cha Kidugala wilayani Wanging’ombe.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Januari 16, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini hapa.

Kamanda Banga amesema mbegu hizo feki zilizokamatwa na jeshi hilo ni aina ya tembo kilo 286 zilizokuwa zikiuzwa kwa wakulima huku wakidanganywa kuwa ni mbegu za chapa hiyo wakati siyo kweli.

Amesema wananchi wa Njombe wamekuwa na uhitaji wa mbegu hivyo matapeli kwa kulijua hilo, wanatumia mbinu mbalimbali kuwatapeli na kujipatia fedha zisizo halali.

“Wanadaiwa kwamba wameshawauzia watu wengi mpaka sisi tunakuja kupata taarifa na kushirikiana na watu wa TOSCI, tayari kuna baadhi ya wakulima wameshazipanda mbegu hizo na hazijaota,” amesema Banga.

Amesema idadi halisi ya watu waliouziwa mbegu hizo feki haijafahamika kwa kuwa wapo wanaotoa taarifa na wengine hawatoi, ila waliofika kituo cha polisi na kuandika maelezo ni wakulima sita.

Amesema jeshi hilo litakapokamilisha uchunguzi wake, watuhumiwa wote watatu watafikishwa mahakamani ili kujibu mashitaka yanayowakabili ya kuuza mbegu feki za mahindi.

Muuzaji na msambazaji wa pembejeo za kilimo mkoani Njombe, Frank Luoga amesema uhaba wa mbegu na mbolea ndiyo unaosababisha wakulima kuuziwa mbegu au mbolea feki.

“Mfano sasa hivi tangu msimu wa kilimo uanze wakulima wanahangaika sana mbegu hakuna, wakati huo wanawapa mianya wahalifu waweze kufanya hivyo” amesema Luoga.

Ameiomba Serikali kuhakikisha pembejeo za kilimo zinapatikana kwa wakati na kuwafikia wakulima, hiyo itapunguza mianya ya watu kutengeneza mbegu na mbolea ambazo hazifai.

Naye Jane Ngenzi mkulima wa mkoani hapa amesema madhara ya mbegu na mbolea feki ni kufifisha nguvu za mkulima za kupata anachokitamani baada ya kuwekeza kwenye kilimo.

“Kilimo ni cha msimu mmoja kwa hiyo akishaharibiwa kwenye huo msimu kwa kupata mbegu feki muda wa kusahihisha tena hana hivyo kwa msimu huo maisha yanakuwa yameshaharibika,” amesema Ngenzi.

Wakati huohuo, Kamanda Banga amesema jeshi hilo linamshikilia Brujo Mapunda mkazi wa Iringa kwa kosa la kuingilia mfumo wa malipo ya fedha kinyume na sheria, na kufanikisha kuiba Sh19.8 milioni kutoka kwenye akaunti ya CRDB ya mfanyabiashara wa Kijiji cha Usuka wilayani Wanging’ombe.

“Kuna utapeli ambao unaendelea wahalifu  wanafika kwa watu na kusema wanapandisha 4G wananchi wetu wamekuwa na tabia ya kuwapatia simu na kuwaruhusu kupandisha hiyo 4G, lakini watu hawa wamekuwa wajanja wanachunguza kwenye simu wanakuta kuna akaunti na kwa bahati mbaya kuna watu wanaweka password (nywila) zao kwenye namba za simu, yule anazigundua na kuanza kuhamisha hela,” amesema Banga.

Related Posts