Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria, Ezekiah Wenje amesema maswali kuhusu matumizi ya fedha za kampeni ya ‘Join the Chain’ yanapaswa kuelekezwa kwa mwenyekiti mstaafu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema.
Kauli yake hiyo, inatokana na kile alichofafanua, Lema na wenzake ndiyo mwasisi na aliyekuwa mwenyekiti wa kampeni hiyo iliyokusanya fedha kutoka kwa makundi mbalimbali ya wananchi.
Wenje anakuja na hoja hiyo, katika kipindi ambacho kumekuwa na maswali mengi yaliyokosa majibu kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Akijibu hilo, Lema amesema ataweka mambo hadharani kesho katika mkutano na waandishi wa habari atakaoufanya Dar es Salaam.
Kampeni ya ‘Join the Chain’ ilizinduliwa Machi 25, 2022 na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Tundu Lissu akiwa uhamishoni nchini Ubelgiji.
Lengo la fedha hiyo, lilikuwa ni kuchangia chama hicho kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanyika kwa mkutano wa baraza kuu wa Aprili 25, 2022.
Wenje ameyasema hayo leo, Alhamisi Januari 16, 2025 katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Amesema kampeni ya ukusanyaji wa fedha hiyo ilikuwa chini ya Lema, Lissu na wengine na dhamira yake ilikuwa kufanya mapinduzi ndani ya Chadema.
Kwa mujibu wa Wenje, fedha hizo zilizokuwa zinakusanywa zililenga kutumiwa kuitisha baraza Kuu na mkutano mkuu wa kuwashawishi viongozi yafanyike mabadiliko.
“Mpango wa siri ilikuwa fedha ile inakusanywa ili kuitishwe mkutano mkuu na baraza kuu la chama, ambayo ajenda yake ingekuwa kuwashawishi viongozi kufanya mabadiliko ya uongozi,” amesema.
Kwa kuwa wakati huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alikuwa mahabusu kwa kesi ya ugaidi, amesema mipango ililenga kumpindua.
Wenje amesema aliposhirikishwa kuhusu mpango huo, alijitenga nao na ndiyo sababu ya kutengana na Lissu aliyedai alikuwa rafiki yake.
Katika mabadiliko hayo, amesema Lissu ndiye aliyepangwa kuwa Mwenyekiti badala ya Mbowe ambaye kwa wakati huo alikuwa mahabusu.
Hata hivyo, amesema kampeni ya ‘Join The Chain’ ilikuwa chini ya uenyekiti wa Lema na ndiye anayepaswa kuulizwa zilipo fedha za kampeni hiyo.
Katika hatua nyingine, amesema hataondoka ndani ya chama hicho kwa sababu ya mtu, kwani hata kujiunga kwake hakumfuata yeyote.
Amesema alijiunga na chama hicho kwa sababu ya itikadi yake, hivyo hakuna anayeweza kumshawishi aondoke kwa namna yoyote.
“Sitaondoka Chadema kwa sababu kuna mtu ameondoka, kwa sababu sikumfuata mtu nilifuata itikadi,” amesema.
Hata hivyo, amesema katika kipindi hicho cha kampeni za uchaguzi wa ndani hataruhusu mtu anayemuunga mkono kumtukana mwingine.
“Leo ukimtukana mtu, kesho anataka kugombea urais, unawezaje kwenda kumsafisha. Yeyote anayeniunga mkono ukimtukana mtu hainifanyi niwe msafi,” amesema.
Akijibu hayo, Lema amesema alionya asitokee mtu atakayezungumza, kwa kuwa wamekaidi na Wenje ameongea kesho atakutana na wanahabari kuweka wazi kila kitu.
“Niliwaonya wasizungumze kulinda heshima yangu kwa brother (kaka) Freeman Mbowe, lakini kwa kuwa wamekaidi nitaongea kesho kila kitu,” amesema.
Lema amesisitiza katika mazungumzo yake hayo ataeleza ukweli wa mengi aliyoyabeba moyoni, akidokeza dhambi haipaswi kukaliwa kimya.