Afariki dunia akijaribu kumuokoa mbuzi kisimani kwa dau la Sh40,000

Arusha. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Arusha limeopoa mwili wa Mbaruku Mussa (41), mkazi wa kata ya Olmoti jijini Arusha, aliyezama kwenye kisima cha maji siku tatu zilizopita.

Mbaruku alitumbukia katika kisima hicho Januari 14, 2025, saa 11 jioni akijaribu kumtoa mbuzi aliyekuwa ametumbukia humo kwa ahadi ya ujira ya Sh40,000, lakini aliteleza na kuzama majini.

 Kisima hicho kinachodaiwa kuwa na urefu wa mita 60 kwenda chini na mita 15 za ujazo wa maji, kimekuwa kikitumika kwa matumizi ya nyumbani.

Akizungumza na Mwananchi Digital, leo Ijumaa, Januari 17, 2025, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Osward Mwanjejele, amesema wamefanikiwa kuopoa mwili huo usiku wa kuamkia leo, Januari 17, 2025, saa tano usiku.

“Januari 14, 2025, saa 11 jioni tulipokea simu kutoka kwa wasamaria wema kuwa kuna mtu amezama kwenye kisima cha maji na haraka tulifika eneo la tukio.

“Tulipofika, tulikuwa na vifaa vya uokozi vya maeneo ya wazi, lakini kisima kina maji na mtu huyo hakuonekana, kwa maana hiyo alikuwa ameenda chini ya maji,” ameeleza.

Amesema kuwa kutokana na askari wake kushindwa kuzama kwenye kina cha maji kwa ukosefu wa vifaa vya kusaidia, iliwalazimu kutafuta mashine za kuvutia maji.

“Kwa kushirikiana na viongozi wa mtaa na kata, tulifanikiwa kuvuta maji huku tukitafuta mwili kwa siku tatu hizi, na bahati nzuri usiku wa kuamkia leo tulifanikiwa kuuopoa,” amesema.

Amesema mwili huo umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali ya rufaa Mount Meru kusubiri taratibu za maziko.

Mbali na hilo, Kamanda Mwanjejele amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika maeneo hatarishi, ikiwemo kwenye visima vya maji na chemba za maji taka ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu.

Wakizungumzia tukio hilo, Diwani wa Olmoti, Rafael Lomwiku, amesema kuwa alipigiwa simu Januari 14, 2025, jioni kuwa kuna mtu ametumbukia kwenye kisima cha mtu wanayemfahamu kwa jina moja la Mkambi.

“Nilikuja hadi eneo la tukio, ndipo nikambiwa kuwa Mbaruku ametumbukia kisimani wakijaribu kutoa mbuzi aliyetumbukia siku mbili zilizopita. Ndio nikaanza kupiga simu polisi kuomba msaada,” amesema.

Shuhuda wa tukio hilo, Mohamed Kawaida, amesema siku hiyo walipata tangazo la dau la Sh30,000 kwa mtu atakayemtoa mbuzi aliyezama kwenye kisima hicho.

“Vijana waliitana mtaani, kila mmoja akasema lake, wengine Sh100,000 na wengine Sh60,000. Baadaye mwenye kisima alitoa Sh40,000 ili mbuzi atolewe.

“Wengine walikataa wakaondoka, lakini baadaye jioni akaja Mbaruku na wenzake wanne, wakakubali dau la Sh40,000 na wakaomba kamba ndefu, ambayo ilishikwa na wenzake kwa juu, na yeye akatumbukia,” amesema.

Amesema baada ya kukaribia kwenye maji, wenzake walisikia kishindo ndani ya kisima, na katika kujaribu kuvuta kamba, ikawa nyepesi ikatoka bila mtu, ndipo wakaanza kumuita Mbaruku bila mafanikio, na huo ndio ukawa mwisho wake.

“Sisi tukiwa hapohapo kijiweni tulishuhudia wenzake wakikimbia, ndipo tukasogea eneo la tukio kuona hakuna mtu anayeonekana. Tukaanza kupiga simu kwa viongozi wa mtaa na kata kuja kutoa msaada,” amesema.

Related Posts