UKIENDA kule Visiwani Zanzibar, mshikaji wetu Ibrahim Hamad ‘Hilika’ ni staa mkubwa sana na mashabiki wa soka pale huwaambii kitu kuhusu jamaa.
Wenyewe kutokana na mahaba ambayo wanayo kwa mshambuliaji huyo wameamua kumpachika jina la utani la straika wa nchi wakimaanisha kuwa pale visiwani hakuna mshambuliaji hatari kumzidi.
Mahaba ya Wazanzibar kwa Hilika hayajatokea kwa bahati mbaya bali ni makali yake ya kufumania nyavu aliyoonyesha akiwa na jezi ya timu ya taifa ya Zanzibar ‘’Zanzibar Heroes’ na timu yake ya zamani ya Zimamoto.
Ameifungia Zanzibar Heroes mabao muhimu katika baadhi ya nyakati na kuna misimu fulani aliongozaga kwa kufunga katika Ligi Kuu ya Zanzibar tena kwa kupachika zaidi ya mabao 20 tena sio mara moja kwamba ingeonekana kama anabahatisha.
Kile alichokifanya katika mechi ya fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Burkina Faso alipofunga bao la kwanza la Zanzibar Heroes, Wazanzibar walikiona sana na ndio maana hata shangilia yake ilikuwa ya kibabe sana akionyesha yeye ndio straika wa nchi.
Changamoto ya Hilika ni moja ambayo ni kutokuwa na makali pindi anapovuka bahari na kuja huku bara kucheza timu inayoshiriki Ligi Kuu ya huku hata pale anapoitwa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’..
Kipindi fulani alichukuliwa na Mtibwa Sugar akashindwa kufurukuta hadi akaamua kurudi Zanzibar ambako aliwaka tena hadi kupelekea kumfanya arudi bara awamu hii akijiunga na Tabora United ambayo pia imeonekana kuwa mfupa mgumu kwake.
Pale Tabora amekuwa hapati nafasi katika kikosi cha kwanza akionekana kuzidiwa kete na Heritier Makambo na Yacouba Songne ambao nao pia wamekuwa wakitendea haki fursa ambayo wanapewa na benchi la ufundi.
Ngoja tumuone safari hii huenda bao lake la fainali kule Pemba kwenye Kombe la Mapinduzi linaweza kutuletea Hilika ambaye alifanya wakazi wa visiwa vya Zanzibar kumpa jina la Straika wa Nchi.