Dar es Salaam. Mawakili wa mwanasiasa mkongwe nchini, Dk Wilbroad Slaa, anayekabiliwa na kesi ya jinai katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wamedai haki ya mteja wao inakandamizwa.
Jopo la mawakili wa Dk Slaa linaloundwa na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, Peter Madeleka, Hekima Mwasipu, Sisty Aloyce na Sanga Melikiori, lifikia hatua hiyo baada ya mahakama kuahirisha usikilizwaji wa shauri la maombi ya Jamhuri ya kuzuia dhamana.
Wameeleza watakwenda Mahakama Kuu kufungua shauri la maombi ya mapitio ili iitishe jalada la kesi hiyo iangalie na kujiridhisha na usahihi wa mwenendo wa shauri hilo, hasa kwa uamuzi huo.
Kesi hiyo ilipoahirishwa kwa mara ya mwisho Januari 13, 2025, mahakama iliamuru pingamizi la upande wa utetezi kuhusu uhalali wa kesi hiyo lingesikilizwa leo Januari 17, sambamba na shauri la maombi ya upande wa mashtaka la kuzuia dhamana ya mshtakiwa. Uamuzi uliotolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki anayesikiliza kesi hiyo.
Alitoa uamuzi huo akikubaliana na hoja za upande wa mashtaka kuwa usikilizwaji wa shauri hilo la maombi ya kuzuia dhamana utafanyika baada ya kutoa uamuzi wa pingamizi la upande wa utetezi dhidi ya uhalali wa kesi hiyo kuwepo mahakamani.
Ametoka uamuzi huo baada ya kusikiliza pingamizi la upande wa utetezi leo Ijumaa Januari 17. Amepanga kutoa uamuzi Januari 23 iwapo kesi hiyo ni halali au si halali kuwepo mahakamani.
Baada ya hakimu kupanga tarehe ya uamuzi, upande wa mashtaka uliomba usikilizwaji wa shauri la maombi ya kuzuia dhamana liahirishwe kusubiri uamuzi wa pingamizi la utetezi.
Kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Issa amedai kwa kuwa katika pingamizi hilo mawakili wa utetezi wanadai kesi imefunguliwa mahakamani isivyo halali si busara kusikiliza maombi yanayotokana na kesi hiyo ambayo uhalali wake unapingwa.
Amedai kupingwa kwa kesi hiyo kuwa si halali kuna athiri hata mamlaka ya mahakama kuisikiliza, akashauri ni busara kusubiri uamuzi wa pingamizi dhidi ya uhalali wa kesi kwanza ndipo shauri la maombi ya kuzuia dhamana lisikilizwe.
Hoja hiyo imepingwa na mawakili wa utetezi, Madeleka na Mwabukusi wakidai ni utaratibu wa kawaida mahakama kusikiliza mashauri yote na kutoa uamuzi kwa pamoja, wakirejea kesi mbalimbali za Mahakama Kuu kuunga mkono hoja hiyo.
Wameeleza mteja wao yuko mahabusu hayuko hotelini, umri wake ni mkubwa na ni mgonjwa. Pia mahakama ilishaelekeza pingamizi lao na maombi ya Jamhuri yatasikilizwa kwa pamoja, hivyo lisikilizwe leo ili kuokoa muda.
“Kama utakubaliana na pingamizi letu maana yake kesi ya msingi itakuwa imekufa na shauri hili la maombi litakuwa limekufa kifo cha asili, lakini kama pingamizi halitafanikiwa basi mahakama itaendela na uamuzi wa shauri la maombi ya kupinga dhamana,” amesema Madeleka.
Awali, hakimu Nyaki aliuhoji upande wa mashtaka ni kwa namna gani usikilizwaji wa maombi hayo kabla ya kutoa uamuzi wa pingamizi dhidi ya kesi ya msingi utakuwa na athari. Pia kama upande huo uko tayari kwa usikilizwaji.
Wakili wa upande huo aliomba ahirisho fupi. Baadaye hakimu Nyaki aliamuru shauri hilo litasikilizwa baada ya kutoa uamuzi wa pingamizi la utetezi kuhusu uhalali wa kesi.
Kutokana na uamuzi huo mawakili wa utetezi walisimama wakilalamika, Mwasipu akisema siyo haki kwa mteja wao ambaye ni mzee na mgonjwa kuendelea kuwa mahabusu bila sababu za msingi. Aliungwa mkono na Mwabukusi na Sanga.
Hakimu Nyaki aliondoka mahakamani mawakili hao wakiendelea kulalamikia uamuzi huo.
Askari wa Jeshi la Magereza walimtoa mshtakiwa kizimbani na kumpeleka mahabusu ya mahakama ili kurudishwa katika Gereza la Keko.
Wakili Madeleka kwa niaba ya jopo la mawakili wa utetezi nje ya mahakama aliwaeleza waandishi wa habari kuwa watachukua hatua za kisheria kupinga uamuzi huo Mahakama Kuu.
Dk Slaa alipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Januari 10 na kusomewa shtaka moja.
Katika kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025, Dk Slaa anakabiliwa na shtaka la kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa X zamani twitter, kinyume cha kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015. Amekana shtaka.
Anadaiwa kutenda kosa hilo, Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikielezwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka:
“Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya… na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa… hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”
Pia anadaiwa kuandika: “Samia toka muda mrefu haangaikii tena maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe.”