Dhana potofu uzazi wa mpango na ukweli wake

Dar es Salaam. Uzazi wa mpango ni uamuzi wa hiari wa mtu binafsi mke/mume au mtu na mwenzi wake kuhusu lini waanze kupata watoto, wazae wangapi, wapishane kwa muda gani, lini waache kuzaa na njia gani ya uzazi wa mpango wangependa kutumia.

Matumizi ya kondomu, vipandikizi, sindano, vidonge, kitanzi na kutoshiriki ngono siku za hatari ni baadhi ya njia zinazotumika kupanga uzazi.

Hata hivyo, kumekuwa na dhana mbalimbali potofu kuhusu uzazi wa mpango, haswa njia za uzazi wa mpango za kisayansi, zinasababisha baadhi ya watu kujenga hofu juu ya matumizi ya njia hizo.

Hata katika utafiti uliofanywa na kuchapishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 2019, umebaini kuwa theluthi mbili ya wanawake wenye uwezo wa kubeba mimba, wenye nia ya kuchelewesha kupata ujauzito au kudhibiti idadi ya watoto huacha kutumia huduma za uzazi wa mpango kwa hofu ya madhara ya huduma hizo.

Utafiti huo uliofanywa katika nchi 36, ulibaini wanawake hao kutokana na hofu hizo hatimaye hujikuta wamebeba mimba zisizotarajiwa.

WHO ilieleza kuwa wanawake hao wanahofia kuwa wakitumia huduma za uzazi wa mpango, wanaweza kupata athari za kiafya pamoja na kutoweza kupata ujauzito baadaye.

“Asilimia 85 ya wanawake walioacha kutumia njia hizo walipata ujauzito katika miaka ya mwanzo. Miongoni mwao waliokumbwa na mimba zisizotarajiwa na kuamua kuzitoa, waliacha kutumia njia za uzazi wa mpango kwa hofu ya afya zao, madhara ya njia hizo na changamoto za matumizi,” unaeleza utafiti huo.

Nyasatu John anasema, katika ukuaji wake alijengewa hofu kuwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango, hasa zile za kisayansi husababisha ugumba pamoja na saratani katika kizazi.

Anasema aliamini hivyo na kutokana na hofu hiyo alijikuta akiingia katika matumizi holela ya vidonge vya dharura vya P2.

“Nashukuru baadaye nilifanikiwa kupata elimu sahihi juu ya njia za uzazi wa mpango, kupitia wataalamu waliofika chuoni, sasa nafurahia maisha,” anasema.

Kwa upande wake, Mwanjaa Juma anasema alijikuta akipata mimba nyingine miezi miwili baada ya kujifungua mtoto wake wa kwanza, baada ya kuamini dhana kuwa mama anayenyonyesha hawezi kupata ujauzito.

Getrude Clement, ambaye ni kijana na Mshauri Jopo la Vijana Washauri kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA Tanzania), anasema katika baadhi ya jamii, hasa za vijijini huwachukulia vijana wanaofuatilia uzazi wa mpango kuwa ni wahuni.

Anasema hata anapojitokeza mtu au taasisi kufundisha vijana kuhusu uzazi wa mpango, huonekana anawafundisha kuanza uhuni mapema.

Anasema moja ya manufaa ya njia hizo ni kuwasaidia vijana kufahamu namna sahihi ya kujitunza na kuwaepusha na mimba zisizotarajiwa zinazoweza kuwa kikwazo cha kutimiza ndoto zao.

Anajitolea mfano yeye binafsi kuwa elimu aliyoipata kuhusu masuala ya uzazi wa mpango, imemsaidia kuweza kuhitimu masomo yake bila kupata mimba zisizotarajiwa.

Rahim Nasser, ambaye ni Ofisa Vijana kutoka taasisi ya Management and Development for Health (MDH) anasema changamoto nyingine katika baadhi ya jamii imekuwa ikiwaweka kando vijana wa kiume katika masuala ya uzazi wa mpango kwa kuona masuala hayo yanawahusu wanawake pekee.

Nasser anasema ni vyema jamii kuondokana na imani hiyo, kwani watoto wa kiume nao wana haki ya kupata elimu na kufahamu kuhusiana na masuala ya uzazi wa mpango, hupunguza mimba za utotoni, zisizotarajiwa na hupunguza unyanyapaa.

“Tuwaelimishe pia watoto wa kiume ili waweze kuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko katika jamii,” anasema Rahim.

Akizungumza na Mwananchi, Mshauri wa Masuala ya Afya ya Uzazi kutoka ya Management and Development for Health (MDH), Dk Charles Mngale anasema baadhi ya watu katika jamii wamekuwa na dhana potofu kuwa matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango, hasa zile za kisayansi husababisha saratani katika mfumo wa kizazi.

Anasema hilo halina ukweli wowote, kwani tafiti mbalimbali za kisayansi zilizofanyika zinaonyesha hakuna uhusiano kati ya njia za uzazi wa mpango na kusababisha saratani ya kizazi.

Dk Mngale anasema dhana nyingine ni kwa baadhi ya wanawake wanapotumia baadhi ya njia za uzazi wa mpango na kushindwa kuona siku zao huamini kuwa damu iliyotakiwa kutoka imejikusanya kwenye kizazi ambayo hubadilika na kuwa uvimbe, ukweli ni kuwa hakuna damu ambayo inakuwa imejikusanya katika eneo la kizazi

Anasema kuna baadhi ya wanawake waliotoka kujifungua wamekuwa wakiamini kuwa kabla ya kuanza kupata hedhi hawawezi kupata ujauzito, hivyo kuchelewa kutumia uzazi wa mpango, hadi watakapoanza kuingia katika mzunguko wa hedhi, jambo linalowaweka katika hatari.

“Huwa tunawashauri baada ya kujifungua ni vizuri kuanza kutumia njia ya uzazi wa mpango, kwani kabla ya kuona hedhi bado wanaweza kupata ujauzito mwingine,” anasema Dk Mngale.

Katika maadhimisho ya kitaifa ya siku ya njia ya uzazi wa mpango 2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Mohammed Mang’una anakiri kuwa dhana potofu ni moja ya vikwazo katika utoaji wa huduma za uzazi wa mpango.

Dk Mang’una anasema kuna haja kwa Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili waweze kuondokana na dhana hizo.

Anasema elimu ya afya ya uzazi ni muhimu, kwani itasaidia kupunguza mimba zisizotarajiwa, itawezesha vijana kujitunza, vilevile kuwaepusha na magonjwa mbalimbali ya zinaa.

Related Posts