DILI la mshambuliaji aliyekuwa Pamba Jiji, George Mpole la kutimikia Singida Black Stars, limefia njiani mara baada ya Kagera Sugar kuizidi kete na kumbeba juu kwa juu mfungaji bora huyo wa Ligi Kuu Bara 2021-2022.
Awali iliripotiwa kwamba Singida ilikuwa na mazungumzo na Pamba ya kumchukua Mpole kwa mkopo wa miezi sita, muda uliosalia kwa mchezaji huyo ndani ya klabu hiyo iliyorejea katika Ligi Kuu msimu huu baada ya kuisotea kwa miaka 23.
Mpole ambaye alisaini mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Pamba baada ya kuachana na FC Lupopo ya DR Congo iliyomsajili mara baada ya kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa Bara akiwa na Geita Gold.
Mshambuliaji huyo ambaye ndani ya duru la kwanza wa ligi amefunga mabao mawili katika mechi 16 ilizocheza timu hiyo, inayoshika nafasi ya 14 katika msimamo na ikiwa ni moja ya timu mbili zilizofunga mabao machache zaidi hadi sasa ikiwa na saba kama iliyonayo Tanzania Prisons ya Mbeya.
Hata hivyo, dili hilo la kwenda Singida, limekufa kimyakimya kabla ya dirisha la usajili kufungwa juzi usiku na yeye kuibukia Kagera Sugar iliyofikia makubaliano nayo na kusaini mkataba.
Mwanaspoti linafahamu, kilichokuwamisha dili la staa huyo wa zamani wa Mbeya City na Geita Gold kwenda Singida ni kutofikia makubaliano ya kimasilahi na Kagera alitumia mwanya huo kumaliza kazi na kumbeba.
Mtendaji Mkuu wa Kagera Sugar, Thabity Kandoro na amelithibitishia Mwanaspoti kuwa, mshambuliaji huyo amejiunga na kikosi hicho kwa muda wa miezi sita.
“Tutakuwa na Mpole kwa muda wa miezi sita na atakuwa nasi katika duru la pili wa ligi, akiendelea kumalizia mkataba na kama tutaridhishwa naye zaidi, basi tunaweza kumuongezea kulingana na makubaliano tutakayoyaingia,” amesema Kandoro.
Kagera ipo nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu kwa sasa, ikiwa imecheza mechi 15, ikishinda mbili, sare tano na kupoteza minane akiwa na pointi jumla ya alama 11.