Dodoma. Kumekucha Dodoma ndivyo unaweza kuelezea jiji hili kwa sasa wakati huu Chama cha Mapinduzi (CCM) kikifanya mkutano mkuu wake.
Mitaa mbalimbali ya Jiji la Dodoma imepambwa kwa bendera za CCM na picha za mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Viongozi wa chama na Serikali, wanachama, makada na mashabiki wa CCM wapo Dodoma kushuhudia pamoja na mambo mengine, uteuzi wa Makamu Mwenyekiti-Bara, ambaye jina lake baada ya kupata baraka kwenye vikao vya Kamati Kuu, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) litapigiwa kura ya kuthibitishwa na wajumbe wa mkutano mkuu.
Mbali na uteuzi huo, pia wanachama watapitisha mabadiliko ya Katiba ya CCM ambayo kwa mujibu wa taarifa za ndani zinaeleza, NEC kwenye kikao chake kilichofanyika leo Januari 17, 2025, kimeridhia baadhi ya mabadiliko hayo ambayo yatakwenda kutumika kwenye mchakato wa uteuzi ndani ya chama kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mabadiliko hayo yametajwa kuwa ni mikakati ya chama hicho kuhakikisha wanachama wengi zaidi wanashiriki kufanya uamuzi kuhusu wanachama watakaopitishwa kuwania nafasi za udiwani, ubunge kupitia chama hicho tawala.
Hata hivyo, kuhusu uteuzi wa makamu mwenyekiti ni kwamba, tofauti na ilivyotarajiwa na wengi kuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia angewasilisha jina hilo kwa wajumbe wa NEC, mambo yamekuwa tofauti.
Habari ambazo Mwananchi limezipata zinadai jina hilo huenda likawasilishwa moja kwa moja kwenye mkutano mkuu unaoanza kesho Januari 18 jijini hapa ama kukaitishwa NEC nyingine mapema asubuhi kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu.
“Ni kweli tumemaliza kikao cha NEC na sasa tuko kwenye maandalizi kwa ajili ya mkutano mkuu. Mpaka sasa hakuna jina lililowasilishwa kwa ajili ya kupata baraza za wajumbe, na huenda likawasilishwa kwenye mkutano mkuu au ikaitishwa NEC ya dharura kesho asubuhi mahsusi kwa hilo jina. Tusubiri tuone itakavyoamuliwa,” kimesema chanzo chetu.
Hata hivyo, wakati jina la makamu mwenyekiti likiwa bado kuwekwa wazi, Mwananchi linafahamu kuwa Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amekuwa akipewa nafasi kubwa kuvaa viatu vya aliyekuwa makamu mwenyekiti aliyeomba kupumzika, Abdulrahman Kinana.
Kwa zaidi ya miezi mitano sasa nafasi ya makamu mwenyekiti (Bara) imekuwa wazi na kwa muda wote huo, jina la Pinda limekuwa kwenye midomo ya makada wa CCM kama mrithi sahihi.
Hata hivyo, baada ya kikao cha NEC ni kama kuna hali ya upepo kubadilika na sasa jina la Stephen Wasira limeanza kusikika kwenye korido za CCM.
Zipo sababu kadhaa kutajwa kwa jina la Wasira ikiwemo kuipa nafasi Kanda ya Ziwa, umahiri wa siasa za majukwaani na kwenye midahalo ambao mwanasiasa huyo mkongwe amekuwa akifanya kwa muda mrefu.
Wasira mbali na kuhudumu nafasi mbalimbali ndani ya CCM na Serikali, kwa sasa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
“Natambua Pinda amekuwa akitajwa kwa muda mrefu kutokana na haiba yake, utulivu na mtu asiye na makandokando. “Amelitumikia Taifa hili kwa weledi mkubwa, uaminifu na kujituma. Ana uzoefu kwa sababu amehudumu kwenye nafasi mbalimbali. Hatuna shaka naye na wanachama wanasubiri kumpa kura kama litaletwa jina lake mbele ya wajumbe,” amesema mjumbe mmoja wa NEC ambaye hakupenda kutajwa jina.
Kwa upande wa kada mwingine wa CCM, amesema Pinda na Wasira wamekuwa wakitajwa zaidi na makada wa chama hicho na kwamba, wapo tayari kupokea jina lolote kati yao litakalowasilishwa.
Amesema CCM ina hazina kubwa ya wanachama wenye haiba, uzoefu na utayari wa kukitumikia chama kwenye nafasi mbalimbali.
“Kuna Pinda na Wasira ndio wanasikika sana kwenye kumrithi Kinana. Lolote linaweza kutokea. Kuna sababu nyingi zinazowafanya kuwa watu sahihi, wana busara, uzeofu na weledi kwenye kazi. Nasikia jina bado na hilo limeongeza joto kuhusu ama Pinda au Wasira. Hapa kuna Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Ziwa ambazo zote ni ngome za CCM.
“Huyu mzee Wasira siyo wa kumuangalia kwa mchezo mchezo, ni mtaalamu wa siasa zote za majukwaani na uchochoroni, hivyo naye ni mtu sahihi kama ilivyo kwa Pinda,” amesema kada mwingine wa CCM kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mabadiliko ya Katiba yaja
Wakati uteuzi wa makamu mwenyekiti ukigonga vichwa, habari mpya ni kuwa wanachama wa CCM wajiandae kwa mabadiliko ya katiba ambayo yatawasilishwa mbele ya wajumbe kwenye mkutano mkuu.
Mwananchi linafahamu kuwa, moja ya ajenda kwenye kikao cha NEC kilichoketi Ikulu ya Chamwino leo ni kuwasilishwa kwa mabadiliko hayo.
Inaelezwa mabadiliko hayo pamoja na mambo mengine, yatahusu utaratibu wa kuwapata wateule wa CCM kwenye nafasi mbalimbali zikiwemo za madiwani na wabunge.
Mabadiliko hayo yanatajwa kuongeza idadi ya wapigakura kwenye kuwapata wateule wa CCM kwenye nafasi hizo, tofauti na ilivyo sasa.
Kwa upande wa ubunge na viti maalumu, idadi ya wapigakura itaongezeka ili kuongeza wigo na kuondoa makandokando hasa madai ya rushwa kwenye mchakato wa kura za maoni.
“Kuna mabadiliko ya katiba yatatangazwa kwenye mkutano mkuu, haya yanakwenda kuthibiti vitendo vichafu kwenye mchakato wa kura za maoni. Idadi ya wapigakura na utaratibu mpya ambao utawekwa wazi. Mchakato ujao utahusisha mabalozi wa nyumba 10 kuwapigia kura madiwani. Kwa mujibu wa katiba ya CCM. Kwa kusikiliza ni mabadiliko yenye tija kwa chama,” amesema mjumbe mwingine huku akieleza kuwa andiko la mabadiliko hayo limewasilishwa na Wasira.
Achana na mabasi mapya takribani 20 yenye rangi na nembo ya CCM zilizotinga na baadhi ya wajumbe jijini Dodoma, tayari wajumbe wa mkutano mkuu ambao kwa mujibu wa Ibara ya 99 (3) ya Katiba ya chama hicho wanatakiwa kuwa takriban 1,875, wameshawasili jijini Dodoma kufanya maamuzi hayo.
Mbali na wajumbe ambao wamewasili jijini Dodoma kwa kutumia usafiri wa treni ya mwendo kasi (SGR) na mabasi maalumu yenye rangi ya chama hicho, pia wageni waalikwa wakiwemo wasanii mbalimbali nchini walifika jijini Dodoma jana Januari 16.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete akiwa ameambatana na mkewe Salma Kikwete waliwasili jana kwa kutumia usafiri wa SGR.
Katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma kumepambwa na mabango makubwa na madogo ya kuwakaribisha wajumbe wa mkutano huo na bendera za CCM.
Eneo la makao makuu ya chama hicho maarufu kama White House, kumeonekana wajumbe wa mkutano huo wakitoka na kuingia huku wafanyabiashara wa sare za CCM wakiwa pembeni mwa jengo hilo.
Hata hivyo, barabara inayopita kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Center (JKCC) kutoka mjini kwenda Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ilikuwa na msongamano mkubwa wa magari kutokana na barabara hiyo kutumika na watu wanaokwenda kwenye ukumbi huo.
“Leo nimelazimika kupita barabara inayokatiza jengo la Ofisi ya Takwimu (NBS) ili kukwepa foleni kubwa katika barabara hiyo inayotumiwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM,” amesema Mkazi wa Iyumbu, Ibrahim Mussa.