Arusha. Watumishi wa Mahakama nchini wametakiwa kuongeza imani kwa wananchi kwa kusimamia utaoji haki ulio sawa ili wananchi watumie Mahakama badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Akizungumza leo Ijumaa, Januari 17, 2025, mkoani Arusha katika mkutano wa baraza la wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Jaji Ilvin Mugeta amesema utendaji katika Mahakama unahusu utoaji haki ambayo ndiyo nguzo kuu ya amani katika nchi yoyote duniani.
“Utendaji wa Mahakama unahusu utoaji haki ambayo ndiyo nguzo ya amani ya nchi yoyote duniani, hivyo ni muhimu kuhakikisha wananchi wanaendelea kuwa na imani na Mahakama ili waitumie badala ya kujichukulia sheria mkononi,” amesema.
Jaji Mugeta amesisitiza umuhimu wa usafi wa mahakimu na watumishi wa Mahakama, akisema imani ya wananchi inalindwa na maadili mazuri ya watumishi hao.
“Imani ya wananchi inalindwa na usafi wa mahakimu ambao wanasimamiwa na tume. Kwa muktadha huo, watumishi wa tume wanapaswa kuwa wasafi zaidi. Kuna baadhi ya watumishi wanaodhani kuwa utumishi wa tume ni sawa na utumishi wa kawaida wa umma. Hii si kweli,” amesema.
Ameongeza kuwa Tume ya Utumishi wa Mahakama inashikilia amani ya nchi, na hivyo watumishi wake wanapaswa kuwa makini na kutunza siri za nyadhifa zao.
“Tume inashikilia amani ya nchi, kwa hiyo nawakumbusha wajibu wenu wa kutunza siri. Kuna taarifa ambazo utazipata kwa nafasi yako ya kazi katika tume, na kutokana na unyeti wake, utapaswa kufa nazo isipokuwa kama umeelekezwa vinginevyo na sheria au mamlaka ya juu,” amesema Jaji Mugeta.
Kuhusu nidhamu, Jaji Mugeta amesema watumishi wanapopata stahiki zao ni lazima watekeleze wajibu wao ipasavyo. Pia amehimiza waajiri kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wanaokiuka sheria na taratibu.
Awali, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Profesa Elisante Ole Gabriel, ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, amesema kuwa moja ya masuala yaliyopatiwa kipaumbele ni matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).
“Tume imeanza kutumia akili mnemba (AI) kuanzia mwaka 2023 katika uratibu wa michakato ya ajira. Kwa sasa, tume inaoongoza kuwa taasisi ya kwanza ya umma kutumia AI katika masuala ya ajira, ikiwemo kufanya usaili kwa njia ya Tehama,” amesema Profesa Gabriel.
Ametoa wito kwa taasisi nyingine za umma kujifunza kutoka tume hiyo, akisisitiza kuwa matumizi ya AI yanaokoa gharama, hasa kwa vijana waombaji wa kazi kutoka mikoa mbalimbali.
Katibu wa Chama cha Serikali Kuu na Afya (Tughe), Mkoa wa Dar es Salaam, Sara Rwezaula, amesifu tume kwa kuzingatia utekelezaji wa sheria na ushirikishwaji wa wafanyakazi, akisema vikao hivyo ni muhimu kwa kupanga mipango na kuimarisha maslahi ya wanachama.
“Vikao hivi ni muhimu kwani kwa pamoja tunajadiliana mipango, maslahi ya wanachama na sisi tunaona ni mfano mzuri na kipekee wamekuwa wabunifu sana hasa kwenye Tehama, wameweza kuwa na mifumo mizuri hasa katika usaili wa waajiriwa wapya,” amesema.