JKT waitana kambini, kocha akilia na mastraika

KIKOSI cha JKT Tanzania kesho Jumamosi kinaanza rasmi kambi ya mazoezi kwa ajili ya kujiweka tayari kumaliza duru la pili la Ligi Kuu Bara, huku kocha wa timu hiyo, Ahmed Ally akilia na safu ya ushambuliaji.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inatangaza mabadiliko ya tarehe ya kurejea kwa michezo ya ligi ambayo hapo awali ilipangwa kuendelea Machi 1, 2025 baada ya kutamatika kwa michuano ya Kombe la Mapinduzi na fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Michezo ya Ligi Kuu  sasa itarejea wiki ya kwanza la Februari kwa michezo ya ‘viporo’ zikiwamo zile za Yanga dhidi ya Kagera Sugar na Simba itakayopepetana na Tabora United mjini Tabora kabla ya kuendelea na michezo ya raundi ya 17.

Tarehe rasmi pamoja na ratiba iliyofanyiwa maboresho, zitatangazwa hivi karibuni na katika kujiweka tayari kwa vita hiyo ya lala salama ya Ligi hiyo, JKT Tanzania iliyotangaza kumnyakua Ally Msengi kutoka TZ Prisons, kuchukua nafasi ya mshambuliaji Danny Lyanga aliyetua Mashujaa, wameitana kambini.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Ahmed Ally alisema baada ya Bodi ya Ligi kutangaza mabadiliko ya ratiba ya kurudi kwa ligi amewataka wachezaji wake kuanza kuripoti mazoezini kesho Jumamosi.

“Jumamosi timu itaanza mazoezi kwaajili ya kujiweka tayari na mechi za duru la pili. Kuhusu usajili ni kweli hatujatangaza mchezaji hata mmoja lakini mimi kama kocha niliandika ripoti ya kuongezewa wachezaji,” alisema Ahmed aliyekuwa akiinoa Kilimanjaro Stars katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 iliyotoka kapa bila bao wala pointi yoyote.

“Niliomba kuongezewa nguvu eneo la ushambuliaji ambalo tayari limepungua baada ya Lyanga kutoka lakini pia kulikuwa na pengo la Charles Ilanfya ambaye aliumia mwanzoni mwa msimu hakuwa sehemu ya kikosi.”

Akizungumzia kurejea kwa ligi mapema tofauti na ilivyokuwa awali kwamba ligi itarudi Machi Mosi alisema kwao kama benchi la ufundi wamefurahia kwasababu walikuwa wanahofia viwango vya wachezaji kuporomoka.

“Ni jambo zuri kwetu kwani kumuacha mchezaji anakaa bila uangalizi wa kocha ni ngumu.”

Related Posts