Kanda ya Ziwa yaongoza matumizi ya televisheni kwa njia ya waya

Dar es Salaam. Licha ya maendeleo ya teknolojia yaliyosababisha watumiaji wengi kuhamia kwenye televisheni za satelaiti (Satellite TV), Kanda ya Ziwa, inayojumuisha mikoa kama Shinyanga, Mwanza, Tabora, Geita na Simiyu, imeonyesha mapenzi makubwa kwa televisheni za waya (Cable TV).

Takwimu kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha Shinyanga inaongoza kwa idadi ya televisheni zilizounganishwa kwa waya, ikiwa na televisheni 4,219 mwaka 2024. Mwanza na Tabora zinafuatia kwa televisheni 2,070 na 1,872 mtawalia.

Idadi ya jumla ya watumiaji wa mikoa ya Kanda ya Ziwa ni zaidi ya nusu ya jumla ya watumiaji wa Cable TV, ambayo ni 16,767. Swali linaweza kuwa, kwa nini televisheni za waya zinapendwa Kanda ya Ziwa?

Miongoni mwa sababu zinazoelezwa ni hali ya uchumi wa watu katika maeneo hayo, lakini pia upatikanaji. Esther Mangula, mkazi wa Chato, anasema, “Upatikanaji wa Cable TV ni rahisi kwangu, ukilinganisha pia na gharama yake kwa mwezi si kubwa kulipa.”

Wakati Kanda ya Ziwa ikionyesha utumaji mkubwa wa Cable TV, upande wa mkoa kama Dar es Salaam, unaongoza kwa kuwa na watumiaji wengi wa televisheni, wao hupendelea dishi na antena.

Kuhusu mawasiliano ya televisheni, mchambuzi wa uchumi, Dk Thobias Swai anasema kukua kwa sekta hiyo kuna matokeo ya pande mbili: “Cable TV zimekuwa chanzo cha habari, kama kuelimisha kuhusu kilimo, lakini pia utabiri wa hali ya hewa katika maeneo hayo. Pia ni chanzo cha ajira kwa mawakala wa usambazaji wa huduma hadi mafundi wanaoweka vifaa hivyo.”

Kuwa na maudhui mazuri zinazowafikia watu wengi zaidi, kwa mfano mambo ya kilimo na pia utabiri wa hali ya hewa, ni msaada mzuri kwa watu hao, pamoja na promosheni nzuri.

Hata hivyo, Swai anaongeza kuwa kuna changamoto. “Iwapo watu hao watatumia muda mwingi kwenye maudhui yasiyo na tija, kutapunguza uzalishaji katika familia na jamii,” amesema.

Related Posts