Kahama. Polisi Mkoa wa Shinyanga limefukua mwili wa Asha Mayenga (62), mkazi wa Lugela, Kata ya Nyamhanga, Manispaa ya Kahama uliofukiwa shambani, baada ya kutoweka kwa siku tano.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Januari 17, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi, amesema mwili huo umekutwa ukiwa umefukiwa jirani na shamba lake la mpunga, lililopo Kijiji cha Malindi, Kata ya Busoka, wilayani humo.
Amesema taarifa za uchunguzi wa awali zinaonyesha mama huyo alikuwa na mgogoro wa shamba na mtoto wake wa kiume.
Kamanda amesema Polisi linamshikilia mtoto wa marehemu na wenzake wawili kwa mahojiano kuhusu tukio hilo.
Kiongozi wa shina namba mbili, Malindi Mtaa wa Seeke, Emanuel Safari amesema alipata taarifa kuwa mama huyo alitoweka nyumbani kwake tangu Jumatatu, Januari 13, 2025.
Safari amesema mama huyo akiwa ameambatana na vijana wake wawili wanaomsaidia kazi walikwenda shambani, baadaye vijana hao walionekana wakirejea peke yao bila mama huyo kuwapo.
Kwa mujibu wa Safari, vijana hao walipoulizwa kuhusu alipo mama huyo walidai aliwakabidhi funguo watangulie kwa ahadi kuwa atarejea nyumbani.
Akizungumzia kubainika kwa mwili huo amesema: “Tukio hili limetokea jana (Januari 16) saa 11:00 baada ya ng’ombe wa Mwana Madutu kuja kuchungwa eneo hili, kutokana na uwepo wa harufu tulihisi kuna kitu,” amesema.
Amesema kutokana na uwepo wa harufu isiyo ya kawaida waliwaita sungusungu, kisha maofisa wa polisi ambao walipofika leo Januari 17 walibaini mwili wa mwanamke huyo ukiwa umefukiwa.
Amesema mwili huo umetambuliwa na umekabidhiwa kwa ndugu na kuzikwa upya.
Mayenga Ng’ombe, mtoto wa marehemu Asha, amedai baada ya ndugu yake (mtuhumiwa) kurejea na kuanza kuhamisha vyombo kwa madai kuwa anahama na kwenda kujitegemea alihisi kuna jambo lisilo la kawaida.
“Nikiwa nyumbani nilimsikia mke wangu anaongea na mdogo wangu akimweleza kuwa mama amepotea, alikuwa ameenda shambani na vijana wawili kulima,” amesema Mayenga.
“Usiku vijana wale walihamisha samani zao za ndani, lakini pia wakaiba mpunga wa marehemu na kwenda kuuza, kisha kupanga chumba katika mtaa mwingine,” amedai.