Mbowe asimulia Lissu, Lema na Heche walivyomuumiza Chadema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameelezea maumivu mbalimbali anayopitia ndani ya chama hicho, akisema hayamkatishi tamaa kwani ndio wito aliouchagua.

Amesema kwa zaidi ya miaka ya 30 akiwa ndani ya chama na miaka 21 ya uenyekiti amepitia mengi, ikiwemo viongozi wenzake waandamizi kumshambulia kwa maneno aliyodai ni ya chuki na hayana ukweli.

Mbowe ni miongoni mwa wagombea watatu wanaowania uenyekiti wa Chadema akiwamo makamu wake bara, Tundu Lissu katika uchaguzi utakaofanyika Januari 21, 2025 ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Mgombea mwingine ni Charles Odero.

Mwanasiasa huyo mkongwe amesema hayo leo Ijumaa, Januari 17, 2025 katika mahojiano maalumu baina yake na wahariri na waandishi wa habari wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL).

Mbowe amezungumzia ukaribu wake na viongozi waandamizi ndani ya chama hicho, Lissu, mjumbe wa kamati kuu, John Heche na waliokuwa wajumbe wa kamati kuu, Godbless Lema na Mchungaji Peter Msigwa.

Lema alikuwa mwenyekiti wa Kanda ya Kaskazini ambaye hakogumbea tena nafasi hiyo huku Mchungaji Msigwa alishindwa kutetea uenyekiti wa Kanda ya Nyasa kwa kushindwa na Joseph Mbilinyi maarufu Sugu.

Katika mahojiano hayo, Mbowe amegusia madai ya  ‘kulamba asali’ akisema wanaomtuhumu hawamjui vizuri akisema anaidai Serikali zaidi ya Sh20 bilioni zinazotokana na uharibifu wa uwekezaji wake wa shamba la kilimo cha kisasa na uvunjwaji wa jengo la Club Bilicanas, mambo aliyosema ni baadhi  tu ya maumivu ambayo anayopitia akiwa Chadema.

Mbowe amemtaja Lema kama miongoni mwa vijana wake wanaomshambulia,   akisema amejiharibia mwenyewe kwa kushindwa kusimamia uongozi wake na sasa amekimbia kugombea uenyekiti wa Kanda ya Kaskazini na ubunge.

Lema aliyejitokeza mbele za waandishi wa habari Januari 14, 2025 na kueleza kiini cha mgogoro ndani ya chama hicho, alimkosoa Mbowe akisema kuwa alikataa kusikiliza ushauri waliokuwa wakimpa.

Mwenyekiti wa Chadema na mgombea wa nafasi hiyo, Freeman Mbowe akizungumza wakati akifanya mahojiano na wahariri na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd yaliyofanyika makao makuu ya MCL jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, Januari 17, 2025.

“Lema ame mishandle (ameshindwa) uenyekiti katika kanda yake, ikafika mahali akawa hataki kugombea uenyekiti wa kanda. Tukamuuliza Lema kwa nini hugombei uenyekiti wa kanda? Yeye anaamini atashughulikiwa, hata kama hutashinda, ni wapiga kura sio mimi,” amesema Mbowe na kuongeza kuwa alichokifanya ni utovu wa nidhamu.

“Bado Lema hajitambui, anaweza kutoka akaita waandishi wa habari, akampiga mwenyekiti, akampiga katibu mkuu, akapiga viongozi wengine, anasahau kwamba mamlaka yake ya nidhamu ni tawi.

“Sasa kila mwanachama nchi hii aite waandishi wa habari, abagaze makamu, katibu mkuu, akibagaze chama, halafu mnamwangalia tu…amesema.

Akifafanua zaidi, Mbowe amesema kwa kipindi cha miaka mitano, Lema ameshindwa kuongoza Kanda ya Kaskazini.

“Hatujawahi kuwa na kiongozi dhaifu wa kanda kama Lema, miaka mitano amekaa pale hakuweza hata kuanzisha hata kamati za kuanzisha kanda.

Waliomkataa Lema sio mimi ni viongozi wa kanda, ni migogoro migogoro, migogoro. Anatoka anashindwa kuwa mwenyekiti wa kanda anaangusha kapu lote kwa Mbowe,” amesema. 

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Lema kujibu madai yaa Mbowe,  amesema baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kanda waliingia kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2019, huku pia akihudhuria kesi zake mahakamani.

“Baadaya uchaguzi wa 2019 hakuna kanda iliyokuwa imeunda hizo kamati, tukaingia kwenye uchaguzi mkuu wa 2020, mambo yakawa magumu tukakimbia wote, mimi Nairobi (Kenya) na baadaye Canada na yeye akawa Nairobi na Dubai.

“Niliporudi mwaka 2023 nilikuta kanda nyingine zimeunda kamati zao Desemba 2022, baada ya miezi mitatu tuliunda kamati, lakini kwa kuwa chama hakikuwa na fedha ni kamati moja tu ilikuwa ikifanya kazi. Hata hivyo, nilifanya operesheni za chama na nilikuwa nikimpa taarifa,” amesema.

Kuhusu  Mchungaji Msigwa ambaye amewahi kumtuhumu kwa kufanya chama hicho kama mali yake binafsi, Mbowe amesema alitofautiana naye kutokana na matusi (ambayo hakuyataja) aliyokuwa akimtusi.

Msigwa aliyesema hayo baada ya kukihama chama hicho kufuatia kushindwa nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Nyasa alipobwagwa na Joseph Mbilinyi maarufu Sugu.

‘’Msigwa alianza kunitukana mapema, yaani miaka mingi sana,’’ amesema Mbowe na kuongeza kuwa wakati huo Sugu ambaye sasa ndiye Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, ndiye aliyekuwa na mvuto.

“Sugu amekuwa mbunge kwa miaka 10, unapuuzaje ushawishi wake? Ni msanii kweli lakini anakubalika kwenye jimbo lake, anagusa wasanii na watu wengi,” amesema.

Katika maelezo yake nyakati tofauti, Msigwa amekuwa akidai kuwa kulikuwa na mkakati wa kuwaondoa kwenye uongozi yeye pamoja na Heche, Lema na Lissu.

“Ilitengenezwa kwamba Msigwa lazima aondoke, Heche aondoke, Tundu Lissu, Lema aondoke kwa hiyo kwa kwanza ikawa natakiwa mimi niondoke,” alisema Msigwa akatika mahojiano yake mtandaoni hivi karibuni.

‘Madai ya kulambishwa asali’

Moja ya hoja ambayo Mbowe amekuwa akishutumiwa na wanachama na viongozi wenzake ni yeye kupewa fedha ‘kulambishwa asali’ na Serikali ili kumfanya kurudi nyuma kwenye harakati za mapambano yake kisiasa.

Miongoni mwa wanaomshutumu ni Lissu ambaye amekuwa anasema Mbowe aliyeingia gerezani na kukaa miezi minane kisha kutoka na kwenda Ikulu kuonana na Rais Samia Suluhu Hassan, ni watu wawili tofauti.

Lissu alisema hiyo ndiyo sababu kubwa iliyomfanya akaamua kugombea uenyekiti.

Mwenyekiti wa Chadema na mgombea wa nafasi hiyo, Freeman Mbowe akizungumza wakati akifanya mahojiano na wahariri na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd yaliyofanyika makao makuu ya MCL jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, Januari 17, 2025.

Katika maelezo yake, Mbowe amesema katika utawala wa awamu ya tano, alipoteza mali ikiwemo uwekezaji kwenye kilimo na amewasilisha vielelezo serikalini akiomba kulipwa.

“Mimi naidai Serikali zaidi ya Sh24 bilioni, nimevunjiwa shamba langu kinyume kabisa cha taratibu, kwenye jengo la Club Bilicanas ambalo uwekezaji wangu ulikuwa asilimia 75 na NHC (Shirika la Nyumba la Taifa) asilimia 25.”

“Sasa mimi Mbowe ambaye nina madai ya Sh24 bilioni, nikipewa hata Sh10 bilioni si ni zangu. Kwa hiyo kila kitu kinachofanyika Mbowe, hata yasiyonihusu wanasema Mbowe. Nimekubali kubeba kila kitu, kutwezwa utu, heshima na  aibu yangu,” amesema Mbowe.

 Lissu kuwania uenyekiti

Akijibu swali alipokeaje hatua ya  Lissu kutangaza kuwania uenyekiti, Mbowe amesema alishaanza kuona dalili za kiongozi huyo kuwania uenyekiti mapema kutokana na kauli zake.

“Sisi wote ni wajumbe wa kamati kuu, mwenzangu ni makamu mwenyekiti wa chama, maamuzi tunayofanya yote tunafanya pamoja, lakini yeye anafanya haya yote hayamhusu. Kwa hiyo hayo yote anakimbia,” amesema.

 “Halafu inafika hatua unasikia makamu yuko Kenya anazungumza na vyombo vya habari, anauliza mbona upinzani ulikuwa na nguvu kubwa Tanzania, mbona sasa umeyumba?” ameeleza Mbowe akizungumzia mahojiano ya Lissu aliyofanya na kituo cha televisheni cha KTN cha Kenya.

“Anaacha kueleza hivi kwamba tumefungiwa, analaumu kwamba tuna uongozi legelege, kwa hiyo tunahitaji uongozi strong (wenye nguvu) ili turudi tulivyokuwa 2015, kwa hiyo anashindwa kueleza madhila….watu kufungwa na yeye mwenyewe kupigwa risasi, watu wameuawa, watu wameenda uhamishoni, yaani hakuona hoja zote hizo, akaona hoja ya kumjibu mtangazaji wa KTN ni moja tu kuwa tuna uongozi dhaifu. 

“Ukishasikia kitu kama hicho unajua tu, Ok kuna ajenda nyingine ya ziada, ni suala la muda tu, kwamba watu wanapiga kelele, hatimaye unakuja kusikia mtu amechukua fomu, mimi haikunishangaza, wala sikushtuka. Nilitegemea na lisingetokea ningeshangaa,” amesema.

Hata hivyo, Mbowe amekiri kufanya vikao na Lissu vya usuluhishi kupitia kwa viongozi wa dini, akisema walilenga kutafuta uhai wa chama na hilo si jambo geni.

“Kwa hiyo haya mambo tuliyazungumza. Unataka kugombea uenyekiti au urais? unafikiri utamaduni unaotumia wa kukanyaga wezako ni sahihi? Sawa unataka kuwa mwenyekiti, sawa hakuna anayekuzuia, lakini unajua athari zake?,” amehoji Mbowe akimwelezea Lissu.

Mbowe ameeleza jinsi mwanasiasa huyo alivyopambana tangu akiwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (Bavicha), akawa Mwenyekiti wa Kanda ya Serengeti hadi aliposhindwa uchaguzi mwaka 2019 na Esther Matiko.

Hata hivyo, amesema alimpa tena nafasi ya ujumbe wa kamati kuu kupitia nafasi zake sita za uteuzi kwa mujibu wa katiba ya chama hicho.

“Mjumbe pekee niliyemchagua kuingia kwenye kamati kuu ni John Heche. Mimi kama mwenyekiti wa chama nina nafasi sita za kuteua wajumbe wa kamati kuu kwa mujibu wa Katiba, lakini ni Heche pekee niliyemteua,” amesema.

Amesema nafasi hizo huwa anazijaza mara chache. Kwa mfano, amesema aliwahi kuwapa Edward Lowasa, Frederick Sumaye, Profesa Mwesiba Baregu na Profesa Abdallah Safari na Mabere Marando kwa nyakati totafuti kulingana na mahitaji.

“Kama haitoshi tulipokuwa tunakwenda kwenye maridhiano, kamati kuu ikaniambia chagua wajumbe wa kwenda nao, nikamchagua tena Heche. Huyu huyu mjumbe wa maridhiano, akitoka anakwenda kutoa taarifa za uongo pembeni, vitu vya uongo kabisa,” amesema.

Akizungumzia madai ya kutaka kumhujumu Heche katika kugombea uenyekiti wa Kanda ya Serengeti, Mbowe amekiri kumshawishi Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Bob Wangwe, lakini akasema hakuwa na lengo baya kwa Heche. 

“Nilikutana na Bob Wangwe, nikamuuliza unagombea nafasi gani? Mbona sijakusikia? Akasema anataka kugombea Tarime Mjini, nikaona ana uwezo kwenye siasa na mimi nikaona tuimarishe kanda hiyo.

“Akasema ngoja niwasiliane na familia, akarudi akasema ofisini kwangu hawajaniruhusu kwa hiyo ngoja nisubiri kwanza,” amesema.

Hata hivyo, amesema Heche alikuwa hajamtaarifu kwamba ana mpango wa kugombea nafasi hiyo.

“Baada ya hapo, mtu anatokwa mapovu, mwenyekiti hamtaki Heche anamwandaa Bob Wangwe, kwa hiyo Wangwe hana sifa? Mara Mbowe anapanga safu, mwenyekiti ni wajibu wangu  kupanga watu wenye sifa,’’ amesema.

Jitihada za kumpata Heche aliyewahi kuwa mbunge wa Tarime Vijijini kuzungumzia alichokisema Mbowe  zimeshindikana.

Mwenyekiti wa Chadema na mgombea wa nafasi hiyo, Freeman Mbowe akizungumza wakati akifanya mahojiano na wahariri na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd yaliyofanyika makao makuu ya MCL jijini Dar es Salaam, leo Ijumaa, Januari 17, 2025.

Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa tatu wa Chadema akitanguliwa na waasisi wenzake, Edwin Mtei na Bob Makani (sasa marehemu) amesema uchaguzi huo kuanzia ngazi ya chini hadi taifa,  imeshuhudiwa minyukano ya kila aina.

Amesema iwapo atachaguliwa tena kuongoza, kitu ambacho atakifanya mapema zaidi ni kuunda tume au kamati ya ukweli na upatanishi, ili kumaliza tofauti zilizopo na kusonga mbele wakiwa wamoja.

“Tukimaliza uchaguzi, tutafuata utaratibu unaofanyika duniani kote kutengeneza mapatano na kutibu majeraha ya uchaguzi.

“Tutatengeneza tume ya ukweli na upatanishi kwa sababu watu wamekanyagana sana. Watu wameumizana sana. Nikichaguliwa, tutaitana na kuzungumza kwani tunahitajiana wote,” amesema Mbowe.

Amesema tume au kamati itakayoundwa itashirikisha watu mbalimbali ndani na nje ya chama hicho lengo ni kuhakikisha kila aliyeumizwa kwa namna moja au nyingine anakubali kumaliza tofauti hizo.

Jambo jingine ambalo Mbowe ameligusia ni kukinusuru chama hicho dhidi ya uchaguzi wa ndani na chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu,  akisema matamanio yake uongozi uwe unakaa madarakani miaka mitatu badala ya mitano.

Amesema suala hilo linaweza kuamuliwa tu na mkutano mkuu na iwapo akichaguliwa atapeleka pendekezo hilo ili lianze mara moja kama litaridhiwa. Lengo ni chama kuwa na muda wa kutosha kujiandaa ili kuepuka hiki kinachoendelea kwa sasa.

Mbowe alikuwa akijibu swali aliloulizwa iwapo muda uliobaki kwenda uchaguzi mkuu Oktoba 2025 unatosha kwa wao kumaliza tofauti zao, kuandaa wagombea kwenda kushiriki kikamilifu uchaguzi huo?.

Mbowe amesema iwapo atashinda tena, atapeleka pendekezo kwa mkutano mkuu kuwa uongozi uwe unakaa miaka mitatu ili kutoa chama nafasi ya kujiandaa kwa chaguzi za serikali za mitaa na uchaguzi mkuu.

“Ikiwa uongozi wa sasa utaingia mwaka 2025, ina maana Januari 2028 tuanze uchaguzi wa ndani ili mpaka Desemba tuwe tumemaliza  ili tuwe na mwaka mmoja wa kujiandaa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa na miaka miwili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ili kuondoka katika hili ambalo limetokea,” amesema Mbowe.

Amesema pendekezo hilo si kwamba anataka lianze kufanyika baada ya kung’atuka 2029 kama atachaguliwa.

 “Mimi Mbowe nataka hilo pendekezo likaanze hata sasa. Nikae miaka mitatu, tuanze chaguzi za ndani,”ameeleza.

Related Posts