Mbowe: Siyo kila ninachozungumza na Rais nitafute kibali

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, amejibu madai yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kuhusu kutowashirikisha mazungumzo aliyofanya na Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kutoka gerezani.

Mbowe ametoa kauli hiyo leo, Ijumaa Januari 17, 2025, akiwa nyumbani kwake Mikocheni, Dar es Salaam, wakati wa mahojiano na Azam TV.

Akijibu madai hayo, Mbowe amesema: “Taarifa kwamba sikusema nilichozungumza na Rais ni umbea. Nikiwa gerezani, Rais alikutana na Makamu Mwenyekiti wangu, Mheshimiwa Lissu, huko Brussels (Ubelgiji).

“Walizungumza na Lissu akamshawishi Rais azungumze na Chadema kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo kunitoa gerezani. Sasa, yeye kuzungumza na Rais ilikuwa haki, lakini mimi, Mwenyekiti wake, kuzungumza na Rais imekuwa jambo kubwa? Hii si sawa kabisa,” amesema Mbowe.

Mbowe amesisitiza kuwa kama Mwenyekiti wa Chadema, ana mamlaka ya kikatiba kuwa kiunganishi kati ya chama na Serikali, na kwamba hawezi kutafuta kibali kila mara anapozungumza na Rais.

“Mimi ndiye msemaji mkuu wa chama, kwa mujibu wa Katiba ya Chadema. Siyo lazima niite mkutano wa wajumbe wote kuomba kibali cha kuzungumza na Rais wa Taifa. Tumeyazungumza haya waziwazi ndani ya chama, na masuala hayo yamefika mwisho,” amesema Mbowe.

Akizungumzia madai kwamba Chadema imekuwa na msimamo legevu dhidi ya Serikali tangu yeye kukutana na Rais Samia, Mbowe amesema hayo ni mawazo ya mtu binafsi.

“Tumeingia kwenye mazungumzo ya maridhiano tangu mwaka 2022. Tukizungumzia Katiba mpya, tumefanya maandamano na makongamano nchi nzima. Kama upande wa pili hawajataka kusikiliza, kumlaumu Mbowe ni jambo la kitoto sana,” amesema Mbowe.

Mbowe pia amegusia madai ya kwamba kulikuwa na juhudi za kupindua uongozi wake wakati alipokuwa gerezani, akisema suala hilo lipo kwa wahusika wa ndani ya chama kukamilisha uchambuzi.

Kauli hizo za Mbowe zimekuja zikiwa zimebaki siku chache kabla ya Chadema kufanya Uchaguzi Mkuu Januari 21, 2025, ambapo Mbowe na Lissu watapambana kuwania nafasi ya Mwenyekiti wa Taifa. Uchaguzi huo umekuwa wa kihistoria kutokana na mijadala mizito ya ndani kuhusu maridhiano na msimamo wa chama dhidi ya Serikali.

Related Posts