KLABU ya Stand United ‘Chama la Wana’ ya Shinyanga iko hatua za mwisho za kumalizana na Kocha wa Fountain Gate Princess, Juma Masoud ili achukue nafasi iliyoachwa wazi na Meja Mstaafu Abdul Mingange.
Mingange aliyeanza msimu huu na Stand iliyopo Ligi ya Championship akiiongoza katika mechi 12 na kushinda saba, sare mbili na kupoteza tatu kabla ya kuiacha ikiwa nafasi ya tatu na alama 23 na kutimkia Songea United, huku timu ikiachwa mikononi mwa kocha msaidizi, Feisal Hau aliyekaimu ukocha mkuu.
Hau aliiongoza timu hiyo ya Stand katika mechi tatu akiwa ametokea Copco FC ya Mwanza na kwa mujibu wa mmoja wa watu wa benchi la ufundi la Chama la Wana ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kuwa tayari Juma Masoud yupo mjini Shinyanga na mchezo wa mwisho ugenini dhidi ya Geita Gold Januari 12, mwaka huu alikuwepo jukwaani.
Alisema kocha huyo ameshamalizana na timu hiyo na inasubiriwa tu kutangazwa rasmi na klabu kwani kwa sasa anaendelea na maandalizi ya kikosi hicho kuelekea mchezo wa mzunguko wa pili dhidi ya Kiluvya United Januari 26, mwaka huu.
“Kocha mpya tayari ameshapatikana ni Juma Masoud yule aliyekuwa Fountain Gate, hata mechi yetu na Geita Gold alikuwepo jukwaani kwa sababu alikuta tayari tumeshaandaa programu zetu kwahiyo hakutaka kuingilia, lakini tupo naye,” kilisema chanzo hicho.
Ofisa Habari wa Stand United, Ramadhan Zorro akizungumzia ishu ya kocha mpya, alisema; “kocha mpya ameshapatikana bado kumtangaza tu ndani ya wiki hii atajulikana, kuna taratibu za mwisho zinamaliziwa.”