Kilosa. Mtoto mwenye umri wa miaka miwili, Shamimu Nasibu, anadaiwa kuibwa wakati akicheza na mwenzake jirani ya nyumbani kwao, kitongoji cha Kisiwani, kijiji cha Tunda, kata ya Kidodi, Mikumi wilaya ya Kilosa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, mtoto huyo aliibwa Januari 15, majira ya asubuhi, wakati akicheza na mtoto mwenzake aliyefahamika kwa jina la Joseph Natalis mwenye umri wa miaka mitatu, wakati mama wa mtoto huyo akiwa ndani.
Kamanda Mkama amesema baada ya mtu huyo asiyejulikana kupora mtoto huyo, alitokomea kwenye mashamba ya miwa, na jitihada za polisi zinaendelea kuhakikisha mtoto anapatikana na yule aliyekusika na uporaji huo naye anapatikana ili sheria ichukue mkondo wake.
“Niwaombe wananchi yeyote mwenye taarifa zitakazofanikisha kupatikana kwa mtoto huyu, tunaomba atufikishie ili tuweze kuzifanyia kazi,” amesema Kamanda Mkama.
Akisimulia namna mtoto wake alivyoporwa, mama mzazi wa mtoto huyo, Halima Halima Omary, amesema siku ya tukio mtoto wake alikuwa akicheza nyuma ya nyumba na mwenzake, lakini baadaye aliwatoa huko nyuma na kuwaweka mbele ya nyumba ili aweze kuwaona vizuri wakati wakicheza.
“Niliwaweka uwanjani ambako kuna kivuli cha mwembe na mimi nikaingia ndani kuendelea na shughuli zangu za usafi na kuandaa chai ya asubuhi, lakini muda wote huo nilikuwa natoka na kuwachungulia. Mara ya mwisho nilipotoka nilimkuta mtoto mwenzake wa kwangu sikumuona, ndipo kazi ya kumtafuta ilipoanza mpaka leo hii ni siku ya tatu sijampata mwanangu,” amesema Halima.
Amesema mpaka sasa bado hafahamu huyo aliyemchukua mtoto wake ana nia gani, kwani amesema mtoto wake ni mdogo na muda mwingi yupo naye nyumbani na kwamba yeye hana mgogoro na mtu yeyote.
“Mimi na mume wangu ambaye ni baba wa mtoto huyu tupo pamoja na tunaendelea kutafuta kwa kushirikiana na watu mbalimbali wakiwemo viongozi wa kijiji na polisi. Namuomba Mungu mwanangu nimpate akiwa hai na afya njema,” amesema Halima.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kidodi, Abdulatif Khaid, amesema tangu siku alipoibwa mtoto huyo, yeye na wananchi wengine wamekuwa wakifanya doria kwenye maeneo mbalimbali yakiwemo kwenye mashamba ya miwa, lakini mpaka leo hajapatikana.
“Mbali ya kufanya doria na uchunguzi, lakini pia niliitisha mkutano wa kijiji kwa dharura agenda ikiwa ni kupotea kwa mtoto huyu. Katika mkutano huo, polisi walikuja na kuna mikakati mbalimbali tumeweka, moja ikiwa ni kuhakikisha wageni wote wanaoingia kwenye vijiji wanatambuliwa na kuorodheshwa ili kuweka kumbukumbu nzuri,” amesema Khaid.
Diwani huyo amesema maazimio mengine ya kwenye mkutano huo ni kuendelea kufanya doria mpaka mtoto huyo atakapopatikana.
Hata hivyo, amewataka wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao hasa wanapokuwa kwenye michezo, lakini pia amewataka kutoa taarifa za watu wanaowatulia mashaka kwenye maeneo yao, hasa wale ambao sura zao ni ngeni, ili kuzuia matukio ya aina hiyo.