SIMBA inaendelea kujifua kwa ajili ya pambano la mwisho la Kundi A la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya CS Constantine ya Algeria, lakini mastaa wa timu hiyo wanapaswa kuwa makini kwani pambano hilo limepewa mwamuzi Celso Armindo Alvação kutoka Msumbiji ambaye ni mwamuzi wa kumwaga kadi.
Mwamuzi huyo atakayesaidiwa pia na waamuzi kutoka nchini humo, ndio watakaoliamua pambano hilo litakalofanyika kesho Jumapili kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam, Simba ikihitaji ushindi ili kumaliza kama kinara wa kundi hilo linaloongozwa kwa sasa na CSC.
Alvacao ndioye atakayesimama kati kupuliza kipyenga na rekodio zinaonyesha mwamuzui huyo katika mechi 21 za kimataifa alizochezesha amemwaga jumla ya kadi 83 ikiwa ni wastani wa kadi 4 kwa kila mchezo, huku za njano zikiwa ni 81 na nyekundu mbili.
Mwamuzi huyo mwenye umri wa miaka 35 amekuwa na kismati na wenyeji kushinda kwani katika michezo hiyo 21, tisa timu wenyeji imeshinda, huku sita ikiwa ni kwa wageni kuibuka na ushindi na nyingine kama hizo zikiisha kwa sare.
Simba kwa sasa inashika nafasi ya pili katika msimamo wa kundi hilo ikiwa na pointi 10, nyuma ya CS Constantine yenye 12 na zote zikiwa zimeshakata tiketi ya robo fainali, isipokuwa mchezo wa Jumapili ni wa kutaka kumaliza fitina baina yao nani awe kinara wa kundi na yupi amalize wa pili.
Kama Simba itamaliza ya pili kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na vigogo waliocheza fainali iliyopita ya michuano hiyo, RS Berkane ya Morocco au watetezi, Zamalek ya Misri kama sio mabingwa wa 2023, USM Alger ya Algeria zinazoongoza makundi ya B, C na D.
Iwapo Simba itamaliza kana kinara itavikwepa vigogo hivyo, lakini itaangukia mikononi mwa ama Stellenbosch ya Agfrika Kusini, Al Masry ya Misri kama sio Enyimba ya Nigeria au ASC Jaraaf ya Senegal au ASEC Mimosas ya Ivory Coast kutegemea na matokeo ya mechi za mwisho za makundi hayo matatu.
Simba imetinga hatua ya robo fainali kwa msimu wa sita kati ya saba katika ushiriki wa michuano ya CAF tangu mwaka 2018-2019, ikiwamo mbili za Shirikisho Afrika na nne za Ligi ya Mabingwa Afrika.