Dar es Salaam. Mwanahabari, Charles Mwita, anadaiwa kufariki dunia baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana.
Mdogo wa marehemu, Nelson Mwita, alipozungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo Ijumaa, Januari 17, 2025 amedai kuwa tukio hilo la kushambuliwa kaka yake limetokea jana, saa 1 usiku katika kata ya Sirari, wilayani Tarime, mkoani Mara.
“Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, wanadai kaka alivamiwa na watu watatu wasiojulikana, kisha wakampiga risasi kadhaa na kutokomea kusikojulikana. Tayari tukio hilo tumeshaliripoti polisi,” amesema mdogo wa marehemu.
“Ni tukio limetokea ghafla, bado familia haijakaa kupanga taratibu za mazishi,” ameeleza mdogo wa marehemu.
Alipotafutwa Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Tarime Rorya, ACP Mark Njera, kuthibitisha tukio hilo, amesema bado hajapata taarifa ya uwepo wa tukio hilo na kuahidi kulifuatilia na kutoa taarifa kamili.
Endelea kufuatilia Mwananchi