Mwili wa kijana mwenye ualbino wakutwa shambani Morogoro

Morogoro. Mwili wa kijana mwenye ualbino, Rashid Mussa (24), umekutwa katika shamba la mtu asiyejulikana, baada ya kutoweka nyumbani kwake kwa siku tatu.

Rashid alitoweka kutoka kijiji cha Kiziwa, Kata ya Kiroka, wilaya ya Morogoro, na mwili wake ulipatikana kwenye shamba hilo, likiwa limetenganishwa na mnazi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, Amesema leo Ijumaa, Januari 17, 2025 kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha chanzo cha kifo hicho ni kuanguka kutoka juu ya mnazi aliokuwa akiupanda.

Hata hivyo, familia ya marehemu imebaki na maswali kuhusu mazingira ya kifo hicho, hususan baada ya kubaini hakuna kiungo chochote kilichotolewa mwilini.

Kaka wa marehemu, Juma Kibwana, maarufu Bonge, amesema aliwasiliana na wasamaria wema baada ya kupokea taarifa kuhusu mwili wa mdogo wake, ambaye alikutwa pembeni ya mti wa muembe, jirani na mnazi.

Kibwana amesema waliona nazi 14, kamba ya kupandia mnazi, na panga, lakini hakukuwa na dalili ya kuibiwa kwa viungo vya mwili.

“Baada ya polisi kufika, tulichunguza mwili wa mdogo wangu. Hakukuwa na viungo vilivyokuwa vimeondolewa, na mwili ulikuwa umeharibika. Baada ya uchunguzi wa daktari, walikabidhi mwili huo kwa familia na tukazika,” amesema Kibwana.

Kama ilivyo kwa familia ya marehemu, maswali yameendelea kutanda hasa kutokana na hali ya maisha ya Rashid, ambaye hakuwa na tabia ya kupanda mnazi kutokana na hali yake ya ngozi ambayo hatakiwi kupata vidonda.

Mama mzazi wa marehemu, Zawadi Fundi, ambaye pia ni mlemavu wa viungo, amesema aligundua kutoweka kwa mtoto wake asubuhi ya Januari 13, baada ya kugundua kuwa mlango wa chumba alicholala ulikuwa umefungwa na kufuli, jambo ambalo halikuwa kawaida yake.

“Sikuwa na uwezo wa kwenda kumtafuta mwenyewe kwa sababu ya ulemavu wangu. Nilimwambia ndugu zake waende kumtafuta, na mwishowe walikuta mwili wake,” amesema Zawadi, ambaye anasema Rashid alikuwa tegemeo katika familia kutokana na hali yake ya ulemavu na ugumu wa maisha.

Habiba Fundi, mama mdogo wa marehemu, amesema familia yao imekuwa ikikumbwa na matukio ya kihalifu, na akielezea masikitiko yake kuhusu kifo cha kijana huyo. Amesema hakuwahi kuhusika na vitendo vya wizi au ugomvi na mtu yeyote.

Kamanda Mkama amesema polisi wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini undani wa tukio hilo.

Related Posts