Handeni. Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linamshikilia dereva wa lori aliyesababisha ajali iliyoua watu 11 na kujeruhi wengine 13.
Ajali hiyo ilitokea Januari 13, 2025, saa 3:30 usiku, katika kijiji cha Chang’ombe, wilaya ya Handeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Januari 16, 2025 katika kituo kidogo cha polisi cha Mkata, Wilaya ya Handeni, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi, amesema dereva huyo amekamatwa baada ya msako mkali uliofanywa na polisi.
Amefafanua kuwa dereva huyo, Baraka Urio, anashikiliwa kwa kusababisha ajali katika barabara ya Segera–Korogwe eneo la Chang’ombe.
Amesema ajali hiyo ilitokea baada ya lori hilo kuwagonga watu waliokuwa kando ya barabara wakitoa msaada kwa abiria wa gari jingine lililopata ajali.
Gari hilo aina ya Tata, lilikuwa limeteleza na kuacha barabara lakini halikusababisha madhara yoyote kwa binadamu.
“Dereva Baraka Urio aliwagonga watu waliokuwa wakitoa msaada kwa abiria waliopatwa na ajali. Tukio hili limeleta majonzi makubwa, na Jeshi la Polisi linahakikisha kuwa hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yake,” amesema Kamanda Mchunguzi.
Ameongeza kuwa dereva huyo alikamatwa akiwa maeneo ya Mkata wilayani Handeni na atafikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria zitakapokamilika.
Watuhumiwa nyara za serikali mbaroni
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limewakamata watu watatu wakazi wa Wilaya ya Handeni kwa tuhuma za kukutwa na nyara za serikali pamoja na silaha za kienyeji.
Kamanda Mchunguzi amewataja waliokamatwa kuwa ni Juma Omari (34), mkazi wa Kitumbi, aliyekutwa na pembe tano za swala, na Mhina Zuberi (65) pamoja na Rajabu Mhina (34), wote wakazi wa Kitumbi. Watuhumiwa hao walikutwa na magobole sita, mitutu 28, vitako vya magobole, na mashine za kutengenezea silaha hizo.
Kamanda huyo amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na juhudi za kudhibiti uhalifu wilayani Handeni na maeneo mengine ya Mkoa wa Tanga. Ametoa wito kwa wananchi wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja, akionya kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
“Tunawataka wananchi wote kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za wahalifu. Jeshi la Polisi lina azma ya kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao unadumishwa,” amesema.