Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi na uhamisho wa viongozi mbalimbali, akiwemo Dk Grace Magembe ambaye ameteuliwa kuwa Mganga Mkuu wa Serikali.
Taarifa ya uteuzi huo imetolewa leo Ijumaa, Januari 17, 2025, na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka na kusainiwa na kusainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Sharifa Nyaga.
Dk Magembe anachukua nafasi ya Profesa Tumaini Joseph Nagu, ambaye uteuzi wake umetenguliwa. Kabla ya uteuzi huo, Dk Magembe alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Pia, Rais Samia amemhamisha Dk Seif Abdallah Shekalaghe kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya.
Aidha, Dk John Anthony Jingu amehamishwa kutoka Wizara ya Afya kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa uteuzi na uhamisho huu umeanza kutekelezwa mara moja.