Sita kunyongwa kwa mauaji ya askari watatu hifadhini

Sumbawanga. Maandiko ya dini yanaeleza anayeua kwa upanga naye huuawa kwa upanga. Hayo ndiyo yanayodhihirika katika hukumu ya kifo dhidi ya wananchi sita walioshtakiwa kwa mauaji ya maofisa watatu wa Hifadhi ya Taifa Katavi.

Katika tukio la mauaji lilitokea sikukuu ya Mwaka Mpya Januari Mosi, 2021, washtakiwa wanadaiwa kuwaua askari watatu, kisha kukata miili ya wawili vipande vilivyowekwa kwenye mifuko ya sandarusi na kuitupa mtoni.

Mwili wa askari mmoja haukupatikana eneo la tukio, ikielezwa huenda uliliwa na wanyama kwa kuwa kilipatikana kipande cha utumbo ambao vipimo vya vinasaba (DNA), vilithibitisha ni kiungo chake.

Waliouawa katika tukio hilo baada ya kuvamiwa na kundi la wananchi wenye silaha waliopinga ng’ombe 100 na kukamatwa ndani ya hifadhi hiyo ni Muhozya Faustine, Ndifini Luhamba au Masai na Luhende Nyerere.

Waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa ni wakazi sita wa Kijiji cha Mabambasi wilayani Mlele mkoani Katavi, Kija Julunga, Ng’ama Chomeleja, Mussa Lufuga, Salum Ngelela, Singu Jilunga na Luteganya Maduka.

Katika hukumu iliyotolewa Januari 16, 2025 na Jaji Deo Nangela wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, washtakiwa Jilala Chomeka, Jilunga Maduka na Tagala Maduka, waliachiwa huru baada ya mashtaka kutothibitishwa dhidi yao.

Jaji Nangela katika hukumu amesema Hifadhi ya Taifa ya Katavi ni moja ya hifadhi zilizo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa) inayozungukwa na vijiji kadhaa kikiwamo cha Mabambasi.

Siku ya tukio, askari hao wakiwa wanatekeleza majukumu yao, walikamata ng’ombe 110 mali ya mshitakiwa wa nane, Lutenganya Maduka, ambao walikuwa wakichungwa kinyume cha sheria ndani ya hifadhi.

Amesema upande wa Jamhuri ulidai kabla ya kukamatwa ng’ombe hao, askari walikuwa wamekamata wengine 100 mali ya mshitakiwa wa kwanza, Maduka na mshtakiwa wa sita, Jilunga.

Kukamatwa ng’ombe hao kunaelezwa kuliwaudhi washtakiwa waliotoa taarifa kwa mshtakiwa wa tisa Tagala Maduka, aliyekuwa kamanda wa mgambo katika eneo hilo, ambaye baadaye aliachiwa huru.

Katika mkutano uliohudhuriwa na wananchi wengi wa Kijiji cha Mabambasi, wakiwamo washtakiwa wote tisa, kulipitishwa azimio la kuvamia Hifadhi ya Taifa ya Katavi kuchukua ng’ombe waliokamatwa.

Ni kutokana na azimio hilo, inadaiwa washtakiwa hao tisa waliingia ndani ya hifadhi kupitia Mto Kavuu wakiwa wamejihami kwa silaha za jadi (mashoka, mikuki, fimbo na nyingine).

Imeelezwa walipoifikia kambi ya askari hao waliwashambulia na kusababisha vifo vyao, kisha waliondoka na ng’ombe wote waliokuwa wakishikiliwa.

Kwa mujibu wa ushahidi wa upande wa Jamhuri, kulifanyika kikao kingine kijijini wakaazimia baadhi ya wananchi warudi eneo la tukio kuichukua miili na kuitupa Mto Kavuun ili kupoteza ushahidi.

Inadaiwa baada ya kufika eneo la tukio walikuta miili ya Muhozya Faustine na Ndifini Luhamba na baadhi ya viungo walivyoamini ni vya mwili wa Luhende Nyerere, ikiaminiwa uliliwa na wanyama wakali hifadhini.

Miili miwili iliyopatikana eneo la tukio, uamuzi ulifikiwa washtakiwa waitupe mtoni, hivyo waliikata vipande na kuiweka kwenye mifuko ya sandarusi (viroba) na kuitupa Mto Kavuu.

Jaji amesema ingawa waliamini kila kitu kimekwenda sawa, hawakujua damu ya mtu hudai kulipiza kisasi kwa kuwa, taarifa za mauaji hayo zilivuka mpaka na kuwafikia polisi katika Kituo cha Inyonga waliofika eneo la tukio la mauaji.

Polisi wakiongozwa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Evodius Kasingwa na maofisa wa Tanapa walipofika eneo la tukio walipata kipande cha utumbo mdogo na mifupa iliyosadikiwa kuwa ya binadamu na suruali ya Muhozya.

Januari 7, 2021 askari F.7940 Koplo Tedson akisaidiwa na Deusdedit Makwala, walichora ramani ya eneo la tukio na baadaye washtakiwa walikamatwa.

Shahidi wa kwanza, SSP Kasingwa alieleza namna alivyopata taarifa za mauaji hayo na kufika eneo la tukio akiwa na maofisa wengine wa polisi ambao walipata utumbo mdogo walioshuku ni wa binadamu na vitu mbalimbali.

Februari 18, 2021, maofisa watatu wa Tanapa walifika ofisini kwake wakiwa na mshtakiwa wa kwanza waliyemkamata kwa mauaji ya askari watatu yaliyotokea ndani ya hifadhi.

Alidai viungo vilivyopatikana eneo la tukio na kuchukuliwa sampuli mbalimbali za DNA majibu yake kutoka Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali yalithibitisha ni vya binadamu.

Kuhusu marehemu Muhozya na Luhamba, shahidi alidai wanaaminika walikufa kwa kuwa miili yao haikuwahi kupatikana hadi alipotoa ushahidi.

Shahidi wa tatu, F.4373 Koplo James, wa tatu G4021 koplo Shauri na wa nne, F. 6408 Sajenti Richard ambao wote ni maofisa wa polisi, walieleza namna walivyoshiriki kukamata watuhumiwa walioshukiwa kutenda mauaji hayo.

Mashahidi wengine ambao ni askari polisi, katika ushahidi wao walieleza namna walivyoandika maelezo ya onyo ya baadhi ya washtakiwa walioeleza walikiri kutenda mauaji hayo na kuwaeleza hatua kwa hatua kile walichofanya.

Kwa upande wao, washtakiwa walikanusha kuhusika na tukio hilo, huku wengine wakisema hawafahamu uwepo wa tukio hilo.

Akitoa hukumu, Jaji Nangela amesema ushahidi katika kesi hiyo uliegemea wa kimazingira kwa kuwa hakuna shahidi aliyeshuhudia mauaji.

Amesema ushahidi kama huo ni lazima uonyesha ni washtakiwa pekee ndio wahusika.

Jaji Nangela kwa kuchambua ushahidi wa mashahidi wa 1,4,6,7,8,10 na 11 na kusoma kilichomo katika vielelezo ambavyo ni maelezo ya onyo ya washtakiwa, hakuna ubishi askari hao watatu waliuawa ndani ya hifadhi.

Kuhusu kama washtakiwa ndio wanaohusika na mauaji hayo, Jaji Nangela amesema upo ushahidi wa askari (marehemu) kukamata ng’ombe mali ya washtakiwa Kija Jilunga, Singu Julunga na Lutegenya.

Hata hivyo, amesema upo ushahidi ambao ni maelezo ya mshtakiwa wa tisa, ambaye baadaye aliachiwa huru na Mahakama, akisema wakati wananchi wanakwenda hifadhini kuchukua ng’ombe, yeye hakwenda ila alijulishwa na mshtakiwa wa kwanza, Kija Maduka kuwa wakati wa kuwakomboa ng’ombe hao, watatu watatu waliuawa.

Amesema kwa maelezo hayo anashindwa kumuunganisha mshitakiwa wa tisa na kosa hilo.

Jaji amesema kupitia ushahidi huo, haoni ushahidi wowote unaomuunganisha mshitakiwa wa saba, Jilunga Maduka na wa pili, Jilala Chomeleka katika kosa hilo, hivyo akaamuru waachiwe mara moja isipokuwa kama wanashikiliwa kwa makosa mengine.

Jaji Nangela amesema ushahidi unaowaunganisha washtakiwa waliobaki ni maelezo yao wenyewe na ya washtakiwa wenzao ambayo yalipokewa kortini.

Amesema mshtakiwa wa tano, Salum Ngelela anaeleza: “Kwa upande ambao mimi nilikuwepo alikimbilia Ndifini Luhamba. Mimi nilimpiga shingoni na ubavuni. Tulimshambulia Ndifini Luhamba mpaka akafa.”

Mshtakiwa wa nne katika maelezo anaeleza: “Katika kambi hiyo tuliwaona watu watatu… miongoni mwao niliwatambua wawili ambao ni Ndifini Luhamba na Luhende Nyerere. Mmoja alivaa sare sikuweza kumtambua.

“Baada ya kufika tu na kutuona, walikimbia. Katika upande niliokuwepo alikimbilia mtu mmoja aitwaye Luhende Nyerere. Mimi nilifanikiwa kupiga sehemu za miguuni kwa fimbo yangu. Binafsi naamini nilimpiga akiwa tayari amekufa.”

Mshtakiwa wa nane katika maelezo yake aliandika: “Faustine Mhozya akiwa chini alilia na kuomba tusimuue. Lufunya Maduka alimchoma tena mkuki eneo la ubavu wake wa kushoto. Alipigwa teke alipojaribu kuinuka na kukaa tena.”

Jaji amesema maelezo ya aina hiyo yanashahibiana kimaudhui ya kile walichofanya, hivyo Mahakama inaona washtakiwa hao sita walikuwa na nia ovu ya kuwaua (askari) marehemu kutokana na silaha walizozitumia katika kufanikisha mauaji.

Ni kwa msingi huo, Jaji amesema adhabu kwa mtu anayepatikana na hatia ya kosa la kuua kwa kukusudia ni moja tu, nayo ni kunyongwa hadi kufa.

Hivyo, washtakiwa hao sita wamepatikana na hatia ya mauaji hayo na wamehukumiwa adhabu ya kifo.

Related Posts