Ukumbi wa moto uchaguzi Bawacha

Dar es Salaam. Haikupita kila nusu saa bila kushuhudiwa ugomvi wa wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) katika Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.

Ugomvi huo kwa sehemu kubwa unasababishwa na hali ya kutoaminiana kati ya wafuasi wa wagombea wa nafasi ya uenyekiti wa baraza hilo.

Wagombea hao ni Celestine Simba na Sharifa Suleiman ambao ndiyo wanaopigiwa kura kwa mara nyingine ili apatikane mshindi wa uenyekiti wa baraza hilo.

Hatua ya kurudiwa kupigiwa kura hizo, inatokana na kukosekana mgombea aliyepata asilimia 50 ya kura zote katika uchaguzi huo, kati ya Celestine, Sharifa na Suzan Kiwanga.

Kwa kuwa Celestine na Sharifa ndio waliokuwa wanaongoza kwa kura kanuni za uchaguzi za Chadema, zinatamka wawili hao wapigiwe kura upya ili apatikane mshindi.

Baada ya wakati huo, hakukuwa na upande uliokuwa unauamini mwingine, kila wakati kuliibuliwa madai ya rushwa na kuingizwa kwa kura feki.

Hali hiyo ilisababisha kupotea kwa utulivu katika ukumbi huo, haikupita kila nusu saa wajumbe ama walirushiana makonde au kutupiana maneno na baadaye wanasuluhishwa.

Katika uchaguzi huo wa marudio, mambo hayakutulia, kwani kuliibuka matukio kadhaa ya kustaajabisha ikiwemo wajumbe wanawake kukutwa kwenye vyoo vya wanaume.

Vitendo hivyo yote, vilihusishwa na rushwa ili kushawishi wajumbe.

Tukio lingine lililoibua tafrani, ni lililohusu mmoja wa wajumbe kuingia ukumbini na pochi iliyodaiwa kuwa na maburungutu ya fedha.

Baadhi ya wajumbe wenzake walishtukia hilo na kuwataka walinzi wamdhibiti asiingie nazo, lakini baadaye aliruhusiwa kuingia.

Hadi saa 5:09 kura za marudio hazikuanza kupigwa na taratibu za kupatikana karatasi zilikuwa zinaendelea.

Related Posts