Vaibu la mashabiki lamuumiza Ahoua

SIMBA inatarajiwa kurudi uwanja wa nyumbani keshokutwa Jumapili kuvaana na CS Constantine ya Algeria, huku kitendo cha kuzuiwa kwa mashabiki wa klabu hiyo kuhudhuria mechi hiyo ya Kundi A ya Kombe la Shirikisho Afrika likimuuliza kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Jean Charles Ahoua.

Nyota huyo anayeongoza kwa mabao na asisti kwa Simba katika michuano hiyo ya CAF na Ligi Kuu Bara, ameliambia Mwanaspoti, wachezaji wa Simba wameumizwa na kuwakosa mashabiki, lakini watajitoa kwa kila njia kuhakikisha wanainyuka Constantine ili waongoze msimamo wa kundi hilo.

Ahoua amesema, adhabu ya kutokuwa na mashabiki kwenye uwanja wa nyumbani imewapunguzia mzuka kwani vaibu lao hasa timu inaposhinda huwa linawakosha Kwa Mkapa.

Simba imefungiwa na Shirikisho la Soka Afrika(CAF) kupitia Kamati ya nidhamu kutokana na vurugu zilizotokea katika mchezo wa pili wa makundi ya michuano hiyo dhidi ya CS Sfaxien ya Tunisia na wekundu hao kushinda kwa mabao 2-1.

CAF imewafungia Simba kucheza bila ya mashabiki kwa mchezo huo, huku ikiwa chini ya uangalizi ili kutorudia kosa kama hilo kama inapaswa kuepuka adhabu kwa mechi ya hatua ya robo fainali ambayo imeingia mapema sambamba na Constantine inayoongoza msimamo wa kundi hilo.

“Tulipoambiwa kuhusu hilo, kila mmoja aliishiwa nguvu, ilikuwa taarifa mbaya kwetu kucheza bila ya watu ambao wanatupa nguvu kubwa kwenye mechi zetu,” amesema Ahoua mwenye mabao mawili na asisti mbili katika hatua hiyo ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho.

“Tunapokuwa uwanjani wakati timu ipo nyuma huwa kuna msukumo wa kujituma huwa unatoka jukwaani au hata tunaposhida lile vaibu la mashabiki lina maana kubwa sana kwetu, lakini safari hii haitawezekana kulipata kwenye mchezo huu,” ameongeza Ahoua aliyefunga mabao saba na asisti tano katika Ligi Kuu iliyosimama tangu mwezi uliopita mwaka jana.

Ahoua ameongeza, licha ya mashabiki kuzuiwa, lakini wataingia katika mchezo huo na malengo yaleyale ya kutafuta ushindi, ili kuongoza kundi lao na kusisitiza endapo watapata ushindi huo itakuwa ni zawadi kubwa kwa mashabiki wao wote ambao wataangaliwa mechi hizo kutoka majumbani kwao au sehemu yoyote ile.

“Hatutapoteza malengo yetu, tutakwenda kutafuta ushindi ambao utakuwa ni zawadi kwa mashabiki wetu, tunajua hawatakuja lakini wataangalia mechi wakiwa kwao huo ushindi utakuwa zawadi kwao.”

Katika mechi ya kwanza dhidi ya Constantine, Simba ilipoteza kwa mabao 2-1 na mechi ya Jumapili itakuwa ni ya kulipa kisasi mbali na mbio za kutaka kumaliza kileleni kwani ikishinda itafikisha pointi 13 na kuwapiku wapinzani wao hao wenye alama 12 kwa sasa kila timu ikicheza mechi tano.

Timu nyingine za kundi hilo ni Bravos do Maquis ya Angola inayoshika nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba na mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo,  CS Sfaxien ya Tunisia iliyotwaa ubingwa mara tatu inaburuza mkia ikiwa haina pointi yoyote licha ya kucheza pia mechi tano kama timu nyingine.

Related Posts