Dar es Salaam. Wakati mchakato wa kuhesabu kura kuwapata viongozi wapya wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) ukiendelea, baadhi ya wanaodaiwa kuwa makada wa chama hicho wanashikiliwa na polisi kwa madai ya kuanzisha vurugu.
Tukio hilo limetokea leo Ijumaa, Januari 17, 2025 wakati kura za wajumbe wa mkutano mkuu, baraza kuu, na viongozi wa Bawacha zikihesabiwa katika ukumbi wa mikutano wa Ubungo Plaza, jijini Dar es Salaam.
Inadaiwa wafuasi hao walianzisha vurugu wakitaka kuingia ndani ya uzio wa ukumbi huo, lakini hawakuruhusiwa kwa sababu si wahusika wa mkutano huo, hatua iliyozua mvutano kati yao na walinzi waliokuwa eneo hilo.
Mwananchi limeshuhudia askari polisi wapatao sita wakiingia kwenye korido za ukumbi huo kupitia mlango mwingine na kwenda moja kwa moja nje ya uzio wa ukumbi kuwakamata wanaodaiwa kuanzisha vurugu na kuondoka nao.
Vurugu zimeanzishwa na wanaume wanaodaiwa kurandaranda nje ya ukumbi walipo wapigakura.
Kutokana na vurugu hizo, baadhi ya wajumbe wa Bawacha wametaka wanaume wanaosimamia uchaguzi huo kupisha, kwani wao wenyewe wanaweza kujisimamia. Wanawatuhumu wanaume hao kuwa chanzo cha vurugu, wakisema wao hawana tatizo lolote, wakihoji kwa nini polisi waitwe kuingilia uchaguzi wao.
Hali hiyo ni mwendelezo wa vurugu zilizotokea usiku wa kuamkia leo Januari 17, ambapo wamedaiwa kufanya uharibifu wa mali za baadhi ya wagombea.
Katika tukio hilo, ugomvi ulizuka watu wakirushiana ngumi nje ya ukumbi wa mkutano. Ugomvi huo ulidaiwa kuhusisha makundi ya upande wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), Tundu Lissu, na ule wa Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ambao wote wanagombea uenyekiti wa chama hicho..