Wadau Shinyanga wataka Serikali ipunguze utitiri wa kodi

Shinyanga. Wadau wa masuala ya kodi mkoani Shinyanga wameishauri Serikali kuondoa utitiri wa kodi kwenye biashara na taasisi ili kupunguza changamoto zinazosababisha baadhi ya wafanyabiashara kukwepa kodi na kushindwa kupiga hatua za maendeleo.

Wadau hao walitoa maoni yao leo Ijumaa, Januari 17, 2025, katika mkutano wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi. Wamesema makato mengi ya kodi yanasababisha Serikali kukosa mapato mengi kutokana na wafanyabiashara kushindwa kuyamudu.

Mfanyabiashara wa viwanda, Gilitu Makula, amesema ushuru wa huduma unawaumiza wafanyabiashara kutokana na kuwepo kwa makato mengi kwenye biashara moja, jambo linalochangia kudorora kwa uchumi wa wamiliki wa biashara hizo.

“Ushuru wa huduma unasababisha migomo ya wafanyabiashara. Tunaomba kuwepo na mfumo mmoja wa ulipaji kodi kwa sababu tunalazimika kwenda ofisi tofauti, kila moja ikitutoza kodi tofauti. Hii ni changamoto kubwa sana,” amesema Makula.

Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) Shinyanga, Laurean Laulenti, ameiomba Serikali kupandisha kiwango kisichokatwa kodi kutoka Sh270,000 hadi Sh500,000 ili kukabiliana na gharama za maisha zinazozidi kupanda.

Laulenti pia amependekeza kiwango cha chini cha kodi kianzie asilimia 5, huku kiwango cha juu kifikie asilimia 20.

Aidha, Mayengo Bageni amependekeza kodi ya mabango kwenye vituo vya mafuta iendelee kutozwa na taasisi moja badala ya sasa ambapo inatozwa na Ewura na Tanroads.

Pia amesema kodi inayolipwa kwa huduma za zimamoto inapaswa kuondolewa, kwa kuwa huduma hiyo inapaswa kutolewa bure kama inavyofanyika kwa Jeshi la Polisi. Amesisitiza haja ya kuwepo kwa taasisi moja inayotoza kodi badala ya taasisi nyingi zinazochanganya wafanyabiashara.

Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Maboresho ya Kodi, CPA Leonard Mususa, amesema tume inaendelea kufanya tathmini ya kina kuhusu mifumo ya kodi ili kuhakikisha kuwa mfumo huo unakuwa rafiki kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.

“Wafanyabiashara wengi hawalipi kodi kwa sababu wanahudumu katika sekta isiyo rasmi. Tume inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kodi inakusanywa kwa njia bora na yenye haki,” amesema Mususa.

Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Julius Mtatiro, amesema Tume ya Rais inazingatia taaluma na weledi wa hali ya juu katika kufanya tathmini ya mifumo ya kodi.

Ameongeza kuwa changamoto za kodi ni changamoto za kitaifa, lakini Serikali inaendelea kufanya juhudi za kuboresha mifumo ya kodi kwa faida ya wananchi na nchi nzima.

Related Posts