Ugonjwa wa kisukari unahitaji udhibiti wa makini wa lishe, kwani chakula kinachochaguliwa na jinsi kinavyoliwa kinaweza kuwa na athari kubwa kwa kiwango cha sukari mwilini.
Hivyo basi, kwa wafanyakazi wenye kisukari wanapaswa kuwa na mpango wa lishe ili kudhibiti hali hii na kuendelea kuwa na afya bora.
Mpango huu unahusisha kula milo mikuu mitatu kwa maana ya chakula cha asubuhi, mchana na cha jioni na milo ya kati, ili kuepuka mabadiliko makubwa ya sukari katika damu.
Kula vyakula vyenye kiwango kidogo cha wanga na vyenye kiasi kidogo cha sukari pamoja na makapi mlo, hii inaweza kusaidia katika kudhibiti kiwango cha sukari kwa ufanisi.
Kisukari kinahusiana na ongezeko la hatari ya matatizo ya moyo. Wafanyakazi wenye kisukari wanahitaji kuepuka vyakula vyenye mafuta mengi na chumvi nyingi, kwani vyakula hivi huongeza hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Mikakati ya chakula inayolenga ulaji wa vyakula vyenye mafuta bora, kama vile mafuta ya mzeituni na vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi kama vile matunda, mboga za majani na nafaka isiyokobolewa inaweza kusaidia kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo.
Moja ya changamoto kubwa kwa wafanyakazi wenye kisukari ni kudumisha uzito wa mwili. Uzito wa mwili usio bora unaweza kuathiri udhibiti wa sukari mwilini.
Kuweka mpango wa chakula unaolenga ulaji wa vyakula vya virutubisho na kuepuka vyakula vyenye kalori nyingi zisizo na virutubisho ni muhimu kwa kudhibiti uzito. Kwa mfano, vyakula vya mboga za majani, matunda, protini jamii ya mbegu kama maharage, ni muhimu kwa kudumisha nishati mwilini bila kuongeza uzito kupita kiasi.
Wafanyakazi wenye kisukari wanahitaji kuwa na nguvu za kufanya kazi. Kula vyakula vyenye virutubisho vya kutosha kama vyakula vya protini, vitamini na madini, ni muhimu kwa kuimarisha nguvu za mwili.
Kuwa na mikakati ya chakula inayojumuisha vyakula vyenye madini ya chuma, vitamini B12 na magnesiamu husaidia kuongeza nguvu na kuepuka uchovu na kupungua kwa utendaji kazini.
Kwa hiyo, wafanyakazi wenye kisukari wanahitaji kuwa na lishe inayotoa nguvu za kudumu na kuepuka kutetereka kwa kiwango cha sukari, ambacho kinaweza kusababisha uchovu.
Wafanyakazi wenye kisukari wanahitajika kuwa na mpango maalumu na thabiti wa lishe ambayo inahusisha vyakula bora na kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya, ili kuishi maisha bora yenye afya na kuepuka changamoto zote zinazoletwa na kisukari.