Watumishi wawili Rombowssa mbaroni wakidaiwa kuomba rushwa ya Sh550,000

Rombo. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Mkoa wa Kilimanjaro inawashikilia watumishi wawili wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo (Rombowssa) kwa madai ya kuomba rushwa ya Sh550,000 kutoka kwa mteja waliyembaini kuwa mita yake ina changamoto.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa, Januari 17, 2025, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo, amewataja watumishi hao kuwa ni Fredrick Mosses Kiwango na Lucas Malaba Vicent.

Chaulo amesema Desemba 31, mwaka 2024, watumishi hao wakiwa katika majukumu yao ya kazi za kawaida za ukaguzi walibaini kuwa mita ya mteja wao ina changamoto iliyosababishwa na mteja huyo na kumchukua na kuondoka naye, na walimtaka atoe faini ya Sh1.5 milioni.

“Desemba 31, 2024 saa 7 mchana, walifika watumishi wawili wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi Rombo (Rombowssa) wakiwa katika kazi zao za kawaida za ukaguzi kwa madai walibaini kuwa mita ya mteja wao ina changamoto iliyosababishwa na huyo mteja, na kumchukua na kwenda naye, walimtaka mteja huyo atoe faini ya Sh1.5 milioni,” amesema Kamanda Chaulo.

Amesema baadaye waliongea na mteja huyo na kumshawishi awape Sh550,000 ili wamalizane, mteja huyo aliwasilisha malalamiko yake Takukuru na ndipo walipomuwekea mtego na kuwakamata.

“Waliongea na huyo mteja na kumshawishi alipe Sh550,000 ili hilo suala limalizike. Januari 10, mwaka huu, mteja huyo aliwasilisha malalamiko yake kwetu, na sisi tuliandaa mtego na kuwakamata wahusika,” amesema Kamanda Chaulo.

Aidha, Kamanda Chaulo amesema watumishi hao watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.

Alipotafutwa Kaimu Mkurugenzi wa Rombowssa, Tumaini Marandu alisema hawezi kulizungumzia suala hilo na kwamba wenye uwezo wa kulizungumzia ni Takukuru wenyewe. 

“Siwezi kulizungumzia suala hili. Tusubiri Takukuru wamalize kazi yao, na sisi ndipo tunaweza kulizungumzia. Hatuwezi kusema kitu ambacho kipo Takukuru,” amesema Tumaini Marandu.

Related Posts