Wawili wafariki dunia kwa kufukiwa mgodini Simiyu

Bariadi. Wachimbaji wadogo wawili wa madini ya dhahabu katika mgodi wa Ikinabusu namba 2, Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, wamefariki dunia baada ya gema kuporomoka na kuwafukia, huku mmoja akinusurika.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Simiyu, Mrakibu Msaidizi wa Zimamoto Faustine Mtitu, akizungumza na waandishi wa habari mjini Bariadi, amewataja waliofariki kuwa ni Mbesa Mayenga (30), mkazi wa Kijiji cha Gilya, na Yombo Yanga (32), mkazi wa Kijiji cha Dutwa. Aliyejeruhiwa ni Mayenga Zegazega (40), mkazi wa Kijiji cha Sapiwi, wote wakiwa wakazi wa Wilaya ya Bariadi.

Ajali hiyo, iliyotokea jana Januari 16, 2025,  saa 10:00 alfajiri, imetajwa kuwa ilisababishwa na uchimbaji holela usiozingatia kanuni za usalama. Kamanda Mtitu amesema wachimbaji hao waliingia kinyemela usiku katika duara lililokuwa limezuiwa kutokana na kutokuwa salama kwa shughuli za uchimbaji.

“Wachimbaji hao waliingia kinyemela usiku katika duara lililozuiwa ili kuchimba dhahabu. Duara hilo halikuwa salama, ndipo gema la udongo lilipoporomoka na kuwafukia, kusababisha vifo vya wawili na kujeruhi mmoja,” amesema Mtitu.

Miili ya marehemu ilitolewa kutoka shimoni na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Somanda mjini Bariadi, huku majeruhi akitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Wachimbaji walioshuhudia ajali hiyo wamesema kuwa kutokuwa imara kwa duara hilo ndicho chanzo cha vifo hivyo, huku wakilaumu wakaguzi wa mgodi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

“Mkaguzi wa mgodi anapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, hasa katika haya maduara yetu. Kutokuwepo kwa uimara wa duara hilo ndiko kulisababisha vifo vya wachimbaji hao,” amesema John Maximilian, mmoja wa wachimbaji waliokuwa eneo la tukio.

Wamesema juhudi za kuwatoa marehemu kutoka shimoni ziligonga mwamba, kwani walikuwa tayari wamefariki dunia walipofikishwa hospitalini.

Viongozi wa mgodi huo hawakupatikana kuzungumzia ajali hiyo, licha ya juhudi za kuwasiliana nao kupitia simu zao za mkononi ambazo hazikupatikana.

Related Posts